Simba, Al Ahly mwendo wa noti tu

Simba, Al Ahly mwendo wa noti tu

Simba inashuka uwanjani leo usiku kuvaana na Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kwa Mkapa, kabla ya kesho watani wao, Yanga kuikaribisha Mamelodi Sundowns, huku mechi zote zikionekana ni mwendo wa fedha kutokana na thamani ya vikosi vya timu hizo nne.


Tuanze na Simba. Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa Transfer Market unaopima thamani ya wachezaji na vikosi unaonyesha Wekundu hao thamani ya kikosi kizima ni Euro 3.78 milioni ambazo ni sawa na Sh 12 Bilioni.


Thamani hiyo ya kikosi kizima cha Simba pale Ahly ni sawa na Mmali wao ghali zaidi kiungo, Aliou Dieng mwenye thamani ya Euro 4.50 milioni ambazo ni zaidi ya Sh 12 Bilioni.


Ahly yenyewe imewaacha mbali Simba, Waarabu hao wakiwa na kikosi chenye thamani ya Euro 32.48 m ambazo ni sawa na sh 88 Bilioni huku Dieng ambaye hatacheza mchezo wa leo kutokana na majeruhi akiwa ndio mwenye thamani kubwa.


Nyuma ya Dieng yumo beki wa kati Mohammed Abdelmonem mwenye thamani ya Euro 30m sawa na sh 8 Bilioni ambaye atakuwepo pale kwenye ukuta. Ndani ya Simba staa mwenye thamani kubwa ni kipa Ayoub Lakred anayesomeka Euro 1.20m sawa na sh 2.75 Bilioni ambapo kipa huyo uhakika ndiye atakayesimama langoni leo.


Nyuma ya Ayoub usimtafute kiungo Clatous Chama bali yumo kiungo Babacar Sarr mwenye thamani ya Euro 500,000 ambazo ni sawa na sh 1.3 bilioni.


Simba imetamba kusaka ushindi wa kishindo kujiweka pazuri katika mechi ya ugenini itakayopigwa wiki ijayo jijini Cairo, Misri na mshindi wa jumla kuvuka nusu fainali.


Hii ni mara ya kwanza kwa Simba na Al Ahly kukutana katika hatua hiyo, lakini zimeshakutana mara nane katika hatua tofauti za michuano ya CAF tangu mwaka 1985 ikianza na Kombe la Washindi, kisha makundi ya Ligi ya Mabingwa mara mbili na African Football League.


Katika mechi zote nane hakuna mbabe, kwani kila moja imeshinda mara tatu nyumbani na kupoteza ugenini na mbili za AFL ziliishia kwa sare ya 2-2 jijini Dar na 1-1 kule Cairo.


Makocha na mastaa wa timu hiyo wameuzungumzia mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi Abongile Tom kutoka Afrika ya Kusini, ambapo beki Shomari Kapombe alikiri mchezo huo ni sapraizi kwa mashabiki na wajitokeze kwa wingi.


Kapombe alisema wamepata muda mzuri wa kujiandaa; “Ni robo fainali yetu ya tano malengo yetu ni kwenda nusu fainali msimu huu hivyo tunapambana kuhakikisha tunavuka hatua inayofuata japo haitakuwa michezo rahisi,” alisema Kapombe, huku Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha akisema Simba inahitaji mabao mengi uwanja wa nyumbani na hakuna kukata tamaa watapambana hadi mwisho.


Benchikha aliongeza kuwakosa baadhi ya nyota waliokuwa timu za taifa katika maandalizi ya kambi Zanzibar, lakini bado hayataathiri chochote.


“Mechi ni kubwa kwa klabu zote mbili na nategemea mambo mazuri na sisi kama Simba tunajua tunacheza na timu kubwa hivyo tumechukua tahadhari zote, matokeo ya kesho yataamua,” alisema Benchikha aliyetwaa taji la Kombe la Shirikisho na CAF Super Cup msimu uliopita alipokuwa na USM Alger akiizingua Yanga na Al Ahly mtawalia kabla ya kuibukia Msimbazi.


Kwa upande wa Ahly, Marcel Koller alisema; “Wachezaji wetu waliopata majeraha Wana umuhimu mkubwa na kutokana na upana wa kikosi chetu naamini kila mchezaji anajiamini na waliopo watafanya vizuri kwenye mechi ya kesho,” alisema Koller.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.