Mbona Yusuf Kagoma katika msimu wake wa kwanza Msimbazi anacheza kama vile amekuwa katika timu kwa miaka lukuki? Anafanya anachokiweza bila hofu kwamba amevaa jezi ya moja kati ya timu mbili kubwa zaidi nchini na ambazo zina mashabiki wengi kila zinapoingia uwanjani. Chasambi na Balua matatizo ni yao wenyewe.
Nipo Afrika Kusini katika michuano ya Cosafa. Kuna vijana kibao ambao hawana majina wapo hapa. Kama Chasambi na Balua wangefanya vizuri inamaanisha kwamba wangekuwa hapa kama mastaa wakubwa dhidi ya vijana wengi ambao wapo hapa achilia mbali Fei Toto na Simon Msuva ambao tunajua ukubwa wao.
Hii ina maana gani nyingine? Nawakumbusha tu wale wapigadebe 😀 ambao wanataka idadi ya wachezaji wa kigeni ipungue katika klabu zetu. Nawakumbusha tu haya mafanikio ambayo tunayashangilia kwa timu zetu katika mechi za kimataifa yanaletwa zaidi na wachezaji wa kigeni. Bila wachezaji wa kigeni sidhani hata kama tungekuwa tunaingia katika makundi achilia mbali kufika robo fainali.
Kinachonishtua zaidi ni kwamba ungesikiliza sifa za kina Chasambi wakati wanakwenda Simba hauoni kama kuna wachezaji wengine wazawa wanaoweza kushika nafasi zao pindi wao wakitolewa kwa mkopo. Ninawatazama wachezaji wawili ambao naweza kuwashikia dhamana ingawa na wao sijui mambo yatakuwa vipi kama wakienda timu kubwa. Navutiwa na Often Chikola wa Tabora United.
Namna anavyotumia mguu wa kushoto huku akicheza winga ya kulia. Sijui kwanini haitwi katika timu ya taifa, lakini hapo hapo nitashangaa kama jina lake halitawekwa katika orodha ya wazawa ambao wanatakiwa na timu kubwa. Hata hivyo, sina uhakika kama hatakuwa Edwin Balua mwingine.
Mwingine ni Idd Kipagwile wa Dodoma Jiji. Huyu aliwahi kucheza Azam. Ana kasi na anajua mpira. Na yeye nikisikia anatakiwa na Yanga au Simba sitashangaa sana. Hata nikisikia Azam wanamtaka tena sitashangaa ingawa sina uhakika kuwa na yeye hatakuwa Chasambi mwingine. Ebu tusubiri. Wakati utatuambia.”
— LEGEND EDO KUMWEMBE.