Kufunga? Tatizo ni washambuliaji wenyewe

Kufunga? Tatizo ni washambuliaji wenyewe


Ukiangalia chati ya wanaowania tuzo ya ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara hivi sasa, kati ya watano wanaoongoza, mshambuliaji wa kati ni mmoja tu ambaye ni Waziri Junior wa KMC.


Wengine wanne katika tano bora hiyo ya wanaokimbiza kwa kufumania nyavu ni viungo ambao ni Stephane Aziz Ki, Feisal Salum, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli.


Vinara wa kufumania nyavu hadi sasa ni Feisal wa Azam FC na Aziz Ki wa Yanga wenye mabao 13 kila mmoja wakifuatiwa na Waziri na mshambuliaji ambaye anaonyesha matumaini katika kinyang’anyiro hicho ni Samson Mbangula mwenye mabao nane.


Ukiangalia mabao mengi ambayo yamepachikwa na wachezaji hao, yamefungiwa ndano ya boksi na ni machache sana yaliyofungwa nje ya eneo la hatari pasipo kujali aliyefunga ni kiungo au mshambuliaji.


Kitendo cha kufungwa kwa idadi kubwa ya mabao ndani ya boksi ni ishara tosha timu zimekuwa zikitengeneza nafasi nyingi za mabao lakini changamoto imekuwa kwa washambuliaji kuzitumia.


Kama zingekuwa hazitengenezi nafasi, isingekuwa rahisi kwa hao viungo kufunga idadi kubwa ya mabao wakiwa ndani ya boksi na badala yake tungeshuhudia mabao mengi ya nje ya eneo la hatari.


Ninachokiona ni kwamba washambuliaji wengi wamekuwa na pupa ndani ya eneo la hatari na hivyo kujikuta wakipoteza nafasi nyingi ambazo wanakutana nazo tofauti na viungo ambao huwa wana utulivu mkubwa wanpolisogelea lango.


Lakini tatizo lingine linalowagharimu washambuliaji ni kutokuwepo katika maeneo sahihi wakati timu inashambulia hivyo mipira mingi inapoanguka ndani ya boksi wao wanakuwa hawapo.


Tuwaambie ukweli washambuliaji wetu kuwa hawazitendei haki timu badala ya kuwafariji kwa hoja za mikimbio na kufungua mabeki sijui.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.