Yanga Kumkatia Rufaa Aucho Bodi ya Ligi

 

Yanga Kumkatia Rufaa Aucho Bodi ya Ligi

Siku moja tu tangu Kamati ya Kusimamia na Kuendesha Ligi ya Bodi ya Ligi (TPLB) kutangaza kumfungia kiungo wa Yanga, Khalid Aucho kwa mechi tatu na kumlima faini ya Sh500,000 kwa kosa la utovu wa nidhamu, mabosi wa klabu hiyo wanadaiwa wapo kwenye mchakato wa kukata rufaa.


Aucho alikumbana na kibano hicho kutokana na kosa la kumpiga kiwiko nahodha wa Coastal Union, Ibrahim Ajibu katika mchezo namba 71 uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.


Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alisema uongozi haujakubaliana na uamuzi huo wa kamati hiyo ya bodi ukiona kiungo huyo amehukumiwa mara mbili.


Gumbo alisema wanaona kamati haijamtendea haki Aucho kwa kuwa tayari alishahukumiwa kwa kupewa kadi ya njano na mwamuzi wa mchezo huo, Emmanuel Mwandembwa baada ya tukio.


“Adhabu hii kwa Aucho imetushangaza sana. Tunaona mchezaji wetu hajatendewa haki kwa kuwa alishaadhibiwa ndani ya mchezo. Hatukuona ulazima tena wa hiki kilichofanyika,” alisema Gumbo na kuongeza:


“Tumemwagiza mwanasheria wetu aitazame hukumu hii kisheria na kama kutakuwa na nafasi ya kukata rufaa kwa adhabu hii, basi afanye hivyo mara moja, tunaona hatujatendewa haki kwenye uamuzi huu.”


Gumbo alisema wanalazimika kutaka rufaa kutokana na kuwa waliwahi kuiandikia Bodi ya Ligi siku za nyuma juu ya beki wa Simba, Henock Inonga aliyefanya kosa kama hilo, lakini walijibiwa mwamuzi alishachukua hatua ndani mchezo kwa kuonyeshwa kadi ya njano, ila safari hii Aucho hilo limesahaulika.


“Tutawakumbusha lile tukio la Inonga alifanya kitu cha hatari sana kwa mchezaji wetu, ingawa mwamuzi alimpa kadi ya njano kama ilivyotokea kwa Aucho ila Yanga tukasema ni adhabu ndogo,” alisema Gumbo.


“Tulipowaandikia barua wenzetu wakatujibu kuwa hawataweza kutoa adhabu mara mbili kwa kuwa mchezaji husika alishapewa adhabu ndani ya mchezo. Tunachojiuliza hili la Aucho mbona sawa na lile tu (la Inonga).”


Yanga italazimika kulipa Sh1 milioni kwa Kamati ya Rufaa na Nidhamu kwa ajili ya kupinga adhabu ya Aucho kulingana na kipengele cha Kanuni za Rufaa 25:1 na ile ya 26(1-6) inayoweka bayana taratibu na ada ya rufaa hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.