Ligi kuu ya Tanzania bara msimu wa 2024/25 imehitimishwa kwa namna isiyo ya kawaida. Yanga SC, klabu yenye historia kubwa na ushawishi mpana katika soka la Tanzania, imetwaa ubingwa wake wa nne mfululizo na wa 31 kwa jumla, baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao Simba SC katika mchezo wa mwisho wa msimu uliofanyika Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa kawaida, ubingwa huleta shamrashamra, sherehe na maadhimisho. Lakini msimu huu, hisia hizo zimepungua kwa kiasi fulani, huku ligi ikimalizika katika mazingira ya sintofahamu, maswali mengi yasiyojibiwa, na kumbukumbu ya mvutano uliohusisha siasa, ushawishi, na sintofahamu ya kiutawala.
Kilichoanza kama sakata la kuahirishwa kwa mechi moja, ile ya dabi ya Kariakoo iliyokuwa ichezwe Machi 8, 2025 kimegeuka kuwa doa kubwa katika uhalali na taswira ya ligi nzima. Mechi hiyo, iliyowekwa kwa ajili ya kuamua mwelekeo wa ubingwa, iliahirishwa kwa mazingira yasiyoeleweka, na ikachezwa takribani miezi minne baadaye.
Licha ya kufungwa kwa pazia rasmi, maswali muhimu yamebaki hewani hasa kuzungumza mchezo wa dabi namba 184. Haya si maswali ya kawaida tu ya soka, bali ni maswali yanayozunguka mamlaka, maamuzi, uwajibikaji, na uadilifu wa taasisi zinazosimamia mchezo huu pendwa.
Kwa nini mechi Iliahirishwa 8? Ripoti iko wapi?
Machi 8,2025 ilikuwa ni siku ambayo macho yote ya Watanzania yalikuwa yameelekezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mchezo wa 184 wa ligi (dabi ya Kariakoo) kati ya Simba na Yanga. Lakini badala ya mpira, taifa likashuhudia sintofahamu isiyoelezeka.
Kwa mujibu wa Simba SC, walinyimwa fursa ya kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja huo siku moja kabla ya mechi, kitu ambacho ni haki yao kwa mujibu wa kanuni. Baada ya hali hiyo, Simba waliamua kutokuingia uwanjani siku ya mechi, wakidai mazingira ya kutokuaminiana na ukiukwaji wa haki zao za maandalizi.
Hali hii ilizua mtafaruku mkubwa mechi ikahairishwa na Bodi ya ligi (TPLB) kuahidi kufanya uchunguzi. Baada ya wiki kadhaa, viongozi wa juu wa TFF, TPLB na vilabu vyote viwili walikutana katika kikao kilichosemwa kuwa “cha suluhu”.
Katika kikao ambacho Yanga waliitwa, Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, alisema wazi kuwa kwenye kikao hicho, mtendaji mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo, alikiri kuwepo kwa ripoti ya kilichotokea Machi 8, lakini pia akaongeza kuwa “ripoti hiyo haijawahi kuwekwa hadharani hadi leo.”
Kwa nini ripoti hiyo haijatolewa? Imefichwa na nani? Nini kilibainika? Je, uchunguzi huu ulikuwa wa kweli au wa kufunika mambo? Haya ni maswali ya msingi ambayo, hadi kufikia mwisho wa msimu, hayapatiwa majibu ya wazi. Katika nchi yenye misingi ya uwazi na uwajibikaji, ripoti kama hii huchapishwa kwa umma. Hapa Tanzania, bado tunasubiri, pengine itatolewa.
Nani alipiga simu kuzuia geti la Uwanja kufunguliwa?
Kabla ya mechi hiyo ya Machi 8, Simba walifika uwanjani Benjamin Mkapa kwa ajili ya mazoezi ya mwisho, lakini kwa madai ya Simba wanasema walizuiwa kuingia. Wakidai kwamba geti la uwanja lilifungwa kwa makusudi, na juhudi za kuingia kwenye uwanja huo kwa ajili ya maandalizi ya mwisho zilikwama kabisa.
Taarifa za ndani zilieleza kuwa sauti za “imani za kishirikina” zilianza kusikika, huku mashabiki na viongozi wa pande zote mbili wakituhumiana kuingiza mambo ya nje ya soka kwenye mchezo. Hakuna kuaminiana. Hali hiyo ilisababisha Simba kupoteza imani na mazingira ya mechi hiyo, wakiamua kutojitokeza kabisa siku ya mechi.
Lakini kilichokuja baadaye ndicho kilichotia doa zaidi. Baada ya kikao cha kujadili hatma ya mechi hiyo, ambayo ilihairishwa na kupangwa Juni 15, 2025 msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, alieleza jambo lililoshtua wapenda soka wa kweli.
“Kwenye kikao chetu tuliuliza pia kuhusu ripoti ya kilichotokea Machi 8, na CEO wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo akakiri kuwa ripoti wanayo na kuna kiongozi mkubwa wa Serikali alipiga simu kuzuia geti la uwanja lisifunguliwe. Lakini hawawezi kumtaja hadharani. Nashangaa hili hajalisema kwenye tuliyoyazungumza leo, tumshauri akiamua kusema aseme yote asibakishe”
Hili ni jambo zito. Kiongozi wa Serikali kupiga simu kirahisi na kuamuru alichoamuru kama ni kweli, ni hatua ya simanzi kwenye soka. Wengi wanatamani kumjua, ni nani huyo aliyetumia mamlaka yake kuzuia maandalizi ya mechi ya ligi kuu? ambaye kwa simu yake, nchi ilizizima na mechi ikachezwa miezi mitatu baadaye.
Mpaka leo, jina hilo halijatolewa. Uamuzi huo haujafafanuliwa. Na hata baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa bodi, Steven Mnguto, na kusimamishwa kazi kwa CEO Almasi Kasongo, bado hakuna kiongozi aliyejitokeza kuthibitisha au kukanusha taarifa hizo.
“Hii ni doa la kiutawala ambalo linapaswa kusafishwa kwa uwazi”, anasema Rahman John, mfuatiliaji wa soka la Tanzania na mshabiki wa Yanga.
Kwanini kanuni hazikufuatwa?
Maelezo ya picha,Aliyekuwa Mwenyekiti wa bodi ya ligi (TPLB), Steven Mnguto (kulia) na Ofisa mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo (kushoto) wamepoteza nafasi zao kwa sababu ya mechi hii ya dabi
Ligi Kuu ya Tanzania Bara inaongozwa na kanuni zinazoeleweka kanuni ambazo zimeandikwa wazi na zinasimamia mwenendo wa kila klabu, wachezaji na maofisa. Miongoni mwa kanuni hizo ni kanuni ya 31 inayosema timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF/TPLB na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu kadhaa.
Ukiacha faini na kulipa fidia ya maandalizi na uharibifu wowote unaoweza kujitokeza, itapokwa alama 15 (kumi na tano)katika msimamo wa Ligi na viongozi waliosababisha jambo hilo watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu. Lakini msimu huu, hali ilikuwa tofauti kabisa.
Machi 8, Simba walitangaza rasmi kuwa hawataingia uwanjani kucheza dhidi ya Yanga, wakieleza kuwa walizuiwa kufanya mazoezi yao ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, haki ambayo inalindwa na kanuni. Walisisitiza kuwa mazingira ya mechi hiyo yalikuwa ya “hila,” na hivyo kukataa kuingia uwanjani.
Juni 15, Yanga nao wakafuata mkondo huo, ikitoa masharti matatu, wapewe ushindi wa Machi 8, hawatacheza mchezo namba 184 dhidi ya Simba katika tarehe yoyote na kamati ya uendeshaji ligi kuu ivunjwe ambayo ilikuwa chini ya Mwenyekiti wa bodi ya ligi (TPLB), Steven Mnguto na Ofisa mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo. Mechi ikafutwa, tena.
Kwa hiyo, katika mechi mbili tofauti, vilabu viwili vikubwa nchini viligoma kushiriki mechi zilizopangwa rasmi. Lakini cha kushangaza hakuna hata kimoja kilichoadhibiwa kwa mujibu wa kanuni. Badala yake, kilichotokea ni viongozi wa bodi ya ligi, kama vile Mwenyekiti Steven Mnguto na Mtendaji Mkuu Almasi Kasongo, kujiuzulu ama kusimamishwa.
Swali kuu linabaki kanuni hizi zinatumiwa kwa nani? Je, timu ndogo za ligi kuu kama KMC au Mashujaa FC wangegoma kwa mazingira haya wangepona dhidi ya kanuni za ligi?
Kwanini marefa wa Misri na je ni suluhu ya ishara ya kutokuaminiana?
Maelezo ya picha,Mwamuzi maarufu kutoka Misri, Amin Mohamed Amin Omar aliitwa kuchezesha dabi ya Kariakoo
Kwa mara ya kwanza katika historia ya ligi kuu ya Tanzania bara, mechi ya ndani ya ligi kuu iliamuliwa na marefa kutoka nje ya nchi. Mechi hii ya Juni 25 kati ya Yanga na Simba ilichezeshwa na mwamuzi maarufu kutoka Misri, Amin Mohamed Amin Omar, akisaidiwa na Mahmoud Ahmed Abo El Regal kama Mwamuzi msaidizi namba moja na Samir Gamal Saad Mohamed ambaye atakuwa msaidizi namba mbili, wote kutokea Misri.
Bila shaka kanuni ya 39(2) ya Ligi kuu Tanzania Bara msimu huu ndio imeipa nguvu kamati ya marefa ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kuwateua marefa kutoka Misri.
Hakuna shaka kwamba hakukuwa na uvunjifu wa kikanuni kwa ujio wa marefa hao. Wachambuzi wa soka wanasema ni vigumu kuiendesha ligi ambayo timu zinahitaji waamuzi wa kigeni ili kushuhudia haki ikitendeka. Hili linaashiria uaminifu umepotea hasa kwenye mechi ya Simba na Yanga. Kwa nadharia hilo linaweza kuwa jibu, ingawa halijathibitishwa na mamlaka zilizoleta marefa hao.
Sasa licha ya sifa walizopewa kwa kutafsiri vizuri sheria za mchezo huo wa Juni 25, uteuzi wao umeibua maswali. Je, ilikuwa ni hatua ya dharura kuondoa mashaka ya upendeleo? Au ni kielelezo cha kutokuaminiana kabisa kwa mfumo wa waamuzi wa ndani?
Pia, hakuna taarifa rasmi kutoka TPLB au TFF kama uamuzi huu utakuwa wa kudumu. Swali kubwa hapa, Je, katika dabi zote zijazo marefa kutoka nje ndiyo watapuliza filimbi? au mazingira tu ya mchezo huu kama na nini hatma ya marefa wa Tanzania