JICHO LA MWEWE: Kelvin John ‘Mbappe’, kuna mahalI amekwama?


JICHO LA MWEWE: Kelvin John ‘Mbappe’, kuna mahalI amekwama?


WASINGEWEZA kujizuia kumuita Kelvin John jina la Mbappe. Waliomuona wakati huo akichomoza katika soka la vijana hapa nchini, walihisi alikuwa na kila sababu ya kupewa jina la utani la Mbappe akilinganishwa na staa wa Ufaransa, Kylian Mbappe.

Kelvin alikuwa na kasi, uwezo wa kuwatambuka mabeki, pia umaliziaji mzuri. Wakati alipotambulishwa kama mchezaji mpya wa Genk niliamini kwamba taifa lilikuwa limepata mchezaji ambaye angekwenda mbali zaidi ya Mbwana Samatta.

Juzi nilikuwa natazama pambano la Taifa Stars dhidi ya Niger pale ugenini Morocco ndipo nilipokumbuka kwamba mara nyingine tena Kelvin alikuwa ameachwa katika kikosi cha Stars. Ni kama mara nne hivi Kelvin hajaitwa katika kikosi cha Stars.

Katika nchi maskini kama hii ambayo haina wachezaji wengi barani Ulaya, Kelvin alipaswa kuitwa achilia mbali kucheza. Sasa hivi hata kuitwa haitwi achilia mbali kucheza. Ina maana hakuna alichomuonyesha Kocha Adel Amrouche.

Sio tu kwamba hakuna alichomuonyesha Amrouche lakini ukweli ni kwamba hata kwa sisi ambao tunamjua tunafahamu kwamba Kelvin huyu sio yule ambaye tulikuwa tunamsubiri akiwa kijana. Sijui ni kitu gani kinatokea kwake, lakini maendeleo yake yamekwenda chini kidogo.

Awali, tulidhani kwamba angeweza kuwa Samatta mwingine katika soka letu, tena angekuwa zaidi. Kwanini? Samatta alitua Genk akiwa na umri wa miaka 23. Ni kitu ambacho anajutia mpaka sasa kwa sababu anaamini kwamba alitua Ulaya kwa mara ya kwanza huku umri ukiwa umesogea.

Kelvin alipata bahati ya kutua Ulaya akiwa na umri wa miaka 18. Juni 2021. Yeye alitua katika mikono salama zaidi akiwa mdogo. Ina maana wazungu walikuwa na nafasi kubwa ya kumkomaza mapema. Kwa sasa ana umri wa miaka 20 na alipaswa kuimarika zaidi kuanzia pale alipokwenda Ulaya.


Umri huu Kelvin alipaswa kuwa ameshajihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Genk kwa maana ya kuanza mechi au kukaa benchi. Hata hivyo, haipo hivyo kwa sasa. Hadi sasa yupo katika hadhi ya kufanya mazoezi katika kikosi cha kwanza lakini sio mchezaji wa kudumu wa kikosi cha kwanza.

Katika kikosi cha timu ya taifa, kama Kelvin angekuwa katika moto ule ule wa soka la vijana alipaswa kuwa anaanza katika kikosi cha kwanza. Labda kwa sababu Samatta bado ana nguvu zake huenda kocha angekuwa anamuweka pembeni mwa uwanja kwa sababu Kelvin yule alikuwa na kasi kubwa.

Haya yote mawili hayatokei. Katika timu yake na katika timu ya taifa. Huku katika timu ya taifa Kelvin angeweza kuwa nahodha ajaye baada ya Samatta. Ndiyo, imekuwa utamaduni wa soka la kisasa katika hizi timu za taifa kwamba mchezaji staa zaidi ndiye anakuwa nahodha wa timu.

Unaweza kuwa na kina Novatus Dismas na Haji Mnoga, lakini mshambuliaji staa zaidi wa nchi anapewa kitambaa cha unahodha. Imetokea hata kwa Mbappe halisi ambaye amepewa kitambaa mbele ya kina Antoine Griezamann.

Nini kinamtokea? Nina wasiwasi na maisha yake binafsi. Kinachopelekwa uwanjani kinatokana na nidhamu kubwa ya kile kinachofanyika nje ya uwanja. Kuna wachezaji ambao wanafurahia kutimiza ndoto zao za kucheza Ulaya halafu kuna wachezaji wanaofurahia zaidi kutimiza mafanikio yao ya kucheza Ulaya.

Siwezi kuhukumu lakini Samatta ana nidhamu kubwa nje ya uwanja. Sijui kama Kelvin anaifuata au vipi lakini nina wasiwasi na hili. Kama angekuwa anafuata hili nadhani sasa hivi angekuwa mbali. Miaka miwili na nusu aliyoishi Ulaya ilitosha kabisa kumpeleka mbali na kuwa mchezaji tegemeo wa Genk na timu ya taifa.

Kuna wakati nilikwenda Genk kumtembelea Samatta na nikafanikiwa kukutana na mastaa wawili wa Genk wa wakati huo. Leon Bailey ambaye kwa sasa yupo Aston Villa pamoja na Wilfried Ndidi ambaye kwa sasa anakipiga Leicester City.

Wakati huo Ndidi alikuwa na miaka 20, huku Bailey akiwa na miaka 18 na tayari wote walikuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Genk ambacho pia kilikuwa kinashiriki michuano ya Europa. Vipi kwa Kelvin ambaye ana miaka 20 kwa sasa?


Nadhani Kelvin ajiangalie kwa makini au wasaidizi wake wamuangalie kwa umakini mkubwa. Bado hajachelewa katika umri wa miaka 20 lakini kucheza kwa mafanikio barani Ulaya kunahitaji nidhamu kubwa ya nje ya uwanja pengine kuliko ile ya ndani ya uwanja.

Sio yeye tu, kuna wachezaji wengi kutoka Afrika ambao maisha ya nje ya uwanja yaliwafanya washindwe kuonyesha vipaji vyao ndani ya uwanja. Unafika Ulaya na kufurahia zaidi maisha ya usiku, maisha ya kuendesha magari ya kifahari, maisha ya kupendwa na wanawake na kadhalika.

Bahati nzuri Kelvin alipokewa Ulaya na Samatta. Ulipaswa kuwa mwanzo mzuri kwake kuendesha maisha yake Ulaya. Ilikuwa bahati kwa sababu Samatta mwenyewe alijipokea mwenyewe Ulaya. Samatta alipaswa kukumbwa na ugonjwa wa kupenda nyumbani (home sickness) kuliko Kelvin ambaye alimpata mtu.

Kelvin bado hajachelewa lakini nimekuwa nikipitia maoni mbalimbali ya Watanzania naona wanaungana na mimi kwamba maendeleo yake ni kama yamekwama mahali. Alipaswa kuwa mbali zaidi kuliko hawa kina Ben Starkie.

Maisha ya wachezaji wetu tunayafahamu wenyewe. Kuna mahali wanashindwa kujikamua zaidi kama ilivyo kwa wachezaji wa Afrika Magharibi. Labda ndio maana mpaka sasa hatuna wachezaji wengine wanaotamba barani Ulaya.

Mwanaspoti

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.