.
Kikosi cha Yanga kinachoendelea kujifua Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam kikijiandaa na mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ugenini dhidi ya CR Belouizdad, kinatarajiwa kuondoka mapema wiki ijayo, huku ikielewa kuwa vigogo kutoka Ubelgiji wamekuja kumfuata Maxi Nzengeli.
Maxi aliyesajiliwa msimu huu kutoka AS Maneama Union ya DR Congo ameanza na moto akifunga mabao saba yakiwamo mawili dhidi ya Simba waliyoipasua 5-1 hivi karibuni, akilingana na Stephane Aziz KI walio sawa na Jean Baleke wa Wekundu wa Msimbazi.
Yanga inatarajiwa kuwa wageni wa CR Belouizdad mjini Algers, Algeria katika mechi ya Kundi D ya Ligi ya Mabingwa itakayopigwa Ijumaa, huku ikielezwa skauti mmoja mzito atatua huko kuwafuata mastaa wawili akiwamo Maxi na Stephane Aziz KI.
Skauti huyo, Alfred Raoul anayefanya kazi na klabu tatu za Ubelgiji atakuwepo kwenye pambano hilo la ugenini ili kuwasoma kwa ufasaha Maxi na Aziz baada ya timu za Eupen na KVK Kortrijk kuonyesha kuvutiwa nao.
Inadaiwa, Kortrijk wao wanataka huduma ya Maxi ambaye wamefichua wamekuwa wakimfutilia kwa muda mrefu kabla hata hajahamia Yanga msimu huu kutoka kwao DR Congo na sasa wanaona ni nafasi ya kumsoma mara ya mwisho kabla ya kufanya uamuzi wa kumbeba jumla wakishazungumza na Yanga.
Raoul ameliambia Mwanaspoti kwa simu kuwa klabu hiyo itamsafirisha yeye (Raoul) sambamba na bosi mkuu wa ufundi kutua Algeria kumtazama kiungo huyo kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza mazungumzo na mabosi wa Yanga.
Kortrijk inayoshika mkia kwenye ligi ya Ubelgiji, lakini bilionea wa timu hiyo, Vincent TAN raia wa Malaysia anataka kukifanyia maboresho kikosi chake ili kukiokoa na janga la kushuka daraja.
“Kortrijk wanamjua Maxi ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, lakini huu mwendelezo wake wa ubora tangu atoke DR Congo ndio kitu kimewarudisha, hivyo Jumatano ya wiki ijayo tutakuwa Algeria na mkurugenzi wa Ufundi wa klabu yao kufanya uamuzi wa mwisho,” alisema.
“Wanataka wachezaji vijana wenye nguvu na kipaji kikubwa unaona nafasi waliyopo kwenye ligi wanataka kutoka kule haraka, hivyo tutajua hukohuko Algeria.”
Raoul aliongeza, mbali na Maxi pia Eupen wamevutiwa na Aziz KI na bosi wao mmoja atatua Algeria kumtazama kwa macho kiungo huyo.
“Eupen hawako kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini wanamtaka zaidi Aziz KI. Wanasema ni mchezaji mwenye akili kubwa hasa pasi zake za mguu wa kushoto, tutakuwa na kiongozi wao mmoja wa juu huko huko Algeria lakini yeye ataungana nasi siku ya Alhamisi,” alisema.
Nyota hao wawili wamefunga mabao 18 yakiwa ni nusu nzima ya mabao yote ya Yanga msimu huu hadi sasa katika mashindano tofauti ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Maxi amefunga mabao tisa, yakiwamo mawili ya CAF ilipoing’oa Asas ya Djibouti.