Hii Hapa ni Jumla ya Fedha Watakazovuna Yanga Baada ya Kuingia Fainali tu

Hii Hapa ni Jumla ya Fedha Watakazovuna Yanga Baada ya Kuingia Fainali tu


 YANGA tayari ipo kwenye fainali za Shirikisho Afrika, baada ya kuwatoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini wiki hii.


Mabingwa hao wa Tanzania, wamejikakikishia kiasi cha Dola 800,000 (zaidi ya Sh 1.8 Bilioni) kwa kutinga fainali na kama itafanikiwa kuinyoosha USM Alger ya Algeria watakaokutana nao basi, itazoa Dola 2 Milioni (zaidi ya Sh 4.7 Bilioni).


Lakini kama unadhani Yanga itavuna kiasi hicho tu, pole yako kwani kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo, tayari wababe hao wameshajihakikisha zaidi ya Sh 700 milioni kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo yaani Benki ya NBC na Azam Media.


Azam inayodhamini matangazo ya ligi hiyo bonasi zake kwa bingwa wa msimu ni Sh 500 milioni, huku kwa NBC wanatoka Sh 100 milioni ilihali wadhamini wakuu wa Yanga, SportPesa inayoipa klabu hiyo zaidi ya Sh 4 Bilioni kwa mujibu wa mkataba mpya walioingia mwaka jana wenye thamani ya Sh 12 Bilioni kwa miaka mitatu, pia itaipa mabingwa hao Sh 150 Milioni kama bonasi ya ubingwa.


Ukiacha fedha hizo za ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kutinga fainali ya CAF, Yanga pia ina uhakika wa kuvuta fedha za maana kutoka kwenye mikataba ya SportPesa na Azam TV ya kurudha maudhi ya klabu hiyo kwenye televisheni ambao ni wa miaka 10 wanye thamani ya ya Sh 41 Bilioni.


Pia Yanga ipo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kwa mujibu wa mkataba wao na SportPesa ikipenya hapo na kutinga fainali itakuwa na uhakika wa kuzoa Sh 75 Milioni na kama italibeba tena kwa msimu wa pili mfululizo itaondoka na Sh 112 milioni kama bonasi.


Kwa hesabu za haraka Yanga kwa msimu huu itavuta zaidi ya Sh 8 Bilioni nane kupitia michuano iliyoshiriki ya Ligi Kuu Bara, ASFC kama itafika mbali na ilipo sasa na kutinga kwake fainali ya CAF mbali na bonasi na fedha za mikataba iliyonayo kupitia Azam TV na SportPesa.


Azam inaipa Yanga kila mwezi Sh 200 milioni kupitia mkataba walioingia nao mwaka juzi ambao unatoa bonasi ya Sh 44.4 kwa miaka 10 kama Yanga ikimaliza bingwa au kushika nafasi ya pili katika ligi kuu ikiwa na maana kwa kubeba ubingwa huo msimu huu imejihakikisha bonasi ya Sh 4.4 bilioni, mbali na SporPesa kutoka kiwango karibia na hicho kwa mkataba wao wenye thamani ya Sh 12 Bilioni kwa mwaka, mbali na udhamini mwingine walionao kwa sasa ukiwamo wa kampuni ya GSM, Haier, Jambo, Maji ya Afya, kiasi cha kuifanya klabu kuishia kishua.


Kama umesahau ni kwamba Yanga imetinga fainali ya CAF kwa kuiondosha Marumo kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kushinda nyumbani 2-0 kisha kutakata ugenini kwa mabao 2-1, lakin ikiwa nusu fainali ya ASFC ikitarajiwa kuvaana na Singida Big Stars Jumapili hii kwenye Uwanja wa Liti, Singida.


Kama itapenya mbele ya Singida inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa kwanza baada ya kupanda ikitumia jina la DTB, Yanga itakwaruzana na Azam FC iliyotangulia mapema fainali kwa kuinyoa Simba kwa mabao 2-1 mechi iliyopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.


Yanga imeingia fainali ya CAF ikiwa timu za Tanzania tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2004 baada ya kuunganishwa kwa michuano ya Kombe la CAF lililoanzishwa mwaka 1992 na aliyekuwa mfanyabishara na mwanasiasa maarufu wa Nigeria, Mashoud Abiola na lile la Kombe la Washindi Afrika lililoanzishwa 1975 na kuwa Kombe la Shirikisho la mfumo wa sasa.


Hata hivyo, Simba ilikuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza fainali za michuano ya CAF 1993 ilipotandikwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast ikiwa nyumbani baada ya awali kutoka suluhu ugenini jijini Abidjan.


Yanga itacheza fainali hizo na USM Alger waliowahi kukutana nao kwenye mechi za makundi ya Shirikisho Afrika mwaka 2018 na kila timu kushinda uwanja wa nyumbani, Yanga ikishinda 2-1 na kupasuka ugenini 4-0 kwenye mechi ya kwanza.


USM ilipata nafasi hiyo kwa kuing’oa ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya kutoka suluhu ugenini na kushinda nyumbani idadi hiyo ya mabao, huku ikiwa na rekodi ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na kufungwa na TP Mazembe ya DR Congo.


Kuhusu mafanikio ya Yanga kwa misimu miwili mfululizo, nyota wa zamani wa timu hiyo, Boniface Ambani alisema siri kubwa kwa vijana wa Jangwani kufanya vizuri ni kutokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya viongozi, wachezaji na benchi la ufundi jambo ambalo anaamini litakuwa silaha nzuri kwao ya kuandika historia mpya nchini.


“Kwanza nawapongeza kwa hatua kubwa na mafaniko waliyofikia, naamini morali iliyopo na kujitoa kwao itakuwa ni chachu ya kuchukua taji la Afrika hivyo waendelee kupambana zaidi ya hapa kwani nafasi wanayo kutokana na umoja uliojengeka miongoni mwao,” alisema Ambani aliyeichezea Yanga msimu wa 2009/2010 na kuibuka Mfungaji Bora wa Bara 2008 akifunga mabao 18.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad