Yanga imetinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo kwa msimu wa pili mfululizo ikiwa ni historia kwa klabu hiyo katika michuano hiyo ya CAF na sasa inasubiri kujua itapangwa na vigogo gani hatua hiyo mara baada ya kufanyika kwa droo Oktoba 7.
Mabingwa hao wa Tanzania ilipenya hatua hiyo baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 7-0 dhidi ya CBE SA ya Ethiopia iliyowafunga kwao bao 1-0 kabla ya juzi usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikiishindilia mabao 6-0.
Ushindi huo kwa Yanga ulipatikana katika mechi za raundi ya pili ya michuano hiyo, baada ya raundi ya kwanza kuifanyia Vital’O ya Burundi kwa kuifunga jumla ya mabao 10-0. Yanga ilishinda kwanza mabao 4-0 kisha kuibuka kidedea tena kwa mabao 6-0.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kuwa miongoni mwa timu 11 za awali kutangulia makundi, huku nyingine tano za mwisho zilikuwa zikitarajiwa kupatikana baada ya mechi za jana za marudiano kisha ndipo droo ya makundi ifuatwe na msakato wa tiketi ya robo fainali ianze kutafutwa kuanzia mwezi ujao.
Kitendo cha Petro Atletico ya Angola kung’olewa juzi imeipa nafasi Yanga kutinga makundi na ijikute ikiangukia katika chungu namba mbili ya droo ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa, huku ikiiweka katika hatari ya kukutana na vigogo vya soka Afrika wakiwamo watetezi, Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na TP Mazembe ya DR Congo vilivyopangwa katika kundi namba moja.
Petro iliyotolewa robo fainali na TP Mazembe ilishtushwa kwa AS Maniema ya DR Congo kwa kutoka suluhu nyumbani na kuchapwa 2-1 ugenini juzi na kuaga michuano hiyo, kitu kimeibeba Yanga kutoangukia chungu namba ya tatu na kuingia cha pili.
Kwa mujibu wa CAF, Yanga imeangukia katika chungu hicho namba mbili sambamba na Pyramids ya Misri anayoitumikia straika wa zamani wa klabu hiyo, Fiston Mayele, Raja Casablanca ya Morocco na CR Belouizdad ya Algeria iliyopangwa kundi moja msimu uliopita na iliyochangia kuivusha kwenda robo fainali na hivyo kuihakikisha Yanga kutokutana na timu hizo tu kati ya 12 inazoweza kupangwa kundi moja.
Mbali na Al Ahly, Eperance zilizovaana katika fainali za msimu uliopita, Mamelodi iliyoing’oa hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti na TP Mazembe iliyowahi kuwanyoosha nje ndani msimu wa 2022-2023 zilipokuwa kundi moja la Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ina nafasi ya kukutana wakali wengine.
Wakali hao ni MC Alger ya Algeria na AS Maniema Union ya DR Congo zilizotupwa chungu namba nne pamoja na Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliyopangwa chungu namba tatu, huku zikisubiri timu nyingine tano za kuungana nazo kwenye vyungu hivyo viwili ambavyo hadi jana mchana vilikuwa havijakamilika.
Katika msimu uliopita katia droo ya makundi ya Ligi hiyo, Yanga ilipangwa chungu namba tatu sambamba na TP Mazembe, Al Hilal ya Sudan, Asec Mimosas ya Ivory Coast na kuangukia Kundi D lililokuwa na Al Ahly, CR Belouizdad na Medeama ya Ghana.
Katika kundi hilo, Yanga ilimaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi nane na mabao tisa ya kufunga na kufungwa sita, nyuma ya Al Ahly iliyoibuka kinara wa kundi hilo ikivuna pointi 12 na mabao sita na yenyewe kufungwa bao moja tu, lililotokana na sare ya 1-1 dhidi ya Yanga jijini Dar es Salaam.
CR Belouizdad yenyewe ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane kama Yanga, ila ikifunga mabao saba na kufungwa sita, lakini matokeo ya jumla baina yao yaliwapa nafasi Yanga kusonga mbele na Medeama ikishika mkia na pointi nne tu ikifunga mabao matatu na kufungwa 12.
Kuvuka kwa Yanga hatua hiyo iliikutanisha na Mamelodi na kutoka nao suluhu katika mechi zote mbili za nyumbani na ugenini kabla ya kupigiana penalti na Wasauzi wakafuzu nusu fainali ilipoenda kukwamishwa na Esperance iliyofika hadi fainali na kupasuka kwa watetezi Al Ahly iliyobeba taji ya 12.