MO DEWJI AINGILIA KATI USAJILI SIMBA SC…SEHEMU ZA MABORESHO ZATAJWA…

MO DEWJI AINGILIA KATI USAJILI SIMBA SC…SEHEMU ZA MABORESHO ZATAJWA…

Baada ya kutokuwa na msimu mzuri wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuwa imeondolewa katika mashindano ya Kombe la FA, Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ anatajwa ameahidi kukabidhi ‘fungu nono’ la fedha kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa usajili wachezaji wenye ubora watakaoisaidia timu hiyo kufanya vyema kwenye michuano mbalimbali msimu ujao, imefahamika.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema Mo ameshaanza kutoa fedha hizo na tayari mchakato wa kuboresha kikosi chao ili kirejeshe heshima na furaha kwa wanachama na mashabiki wake.

Chanzo chetu kimesema kikosi maalum kilichopewa jukumu la usajili na kutafuta wachezaji bora kwa viwango vya juu wameshaanza kazi.

Hata hivyo chanzo hicho kilisema Mo aliwaambia wazi viongozi wa klabu hiyo haridhishwi na viwango vya wachezaji na mwenendo wa timu uliopo kwa sasa, na anataka kuona ‘unyonge’ huo unamalizika.

“Hivi karibuni Bosi alifanya kikao na viongozi wa Simba lakini pia alikutana na washauri wake ili kujadili mwelekeo wa jinsi ya timu yetu inavyokwenda. Ameona madhaifu na bahati nzuri amezungumza na Benchikha (Abdelhak) na kumweleza anaumizwa na mwenendo wa timu, amewapa watu maalum jukumu la kufanya usajili, kufuatilia wachezaji ambao anahitaji ili kuboresha kikosi,” kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza mbali na kufanya maboresho, pia wako tayari kuuza

wachezaji wao ambao watatakiwa na timu nyingine za ndani na nje ya Tanzania.

“Baadhi ya wachezaji watauzwa na wengine tutaachana nao, hapa mezani tuna ofa Henock Inonga, anatakiwa na FAR Rabat ya Morocco,” chanzo hicho kiliongeza.

Alisema pia nafasi ambazo wanataka kuziboresha ni mabeki wawili wa kati, kiungo, winga na washambuliaji.

“Bosi amedhamiria kusimamia kwa karibu mchakato wa usajili, anataka kuona wachezaji wenye ubora na kiwango kizuri wanatua kuja kusaidia timu, tufanye vizuri katika mashindano yote ya msimu ujao. Kushindwa kufikia malengo ya kucheza nusu fainali na kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi, kuondolewa kwenye kombe la FA ni moja ya sababu ya bosi (Mo) kufanya kikao na viongozi wa klabu na washauri wake ili kujipanga upya,” aliongeza mtoa habari huyo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alikiri ni kweli kikosi chao kinahitaji maboresho lakini kwa sasa nguvu na akili zimeelekezwa katika kuhakikisha wanafanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu iliyobakia.

Ahmed alisema wanahitaji kupambana ili kumaliza msimu katika nafasi ya pili na watafikia malengo hayo kwa kufanya vizuri kwenye mechi zote zilizosalia.

“Ni kweli maboresho yatafanyika tena maboresho makubwa, tutajenga timu imara, kwa sasa tunatakiwa tujikite zaidi katika michezo iliyosalia ya ligi kwa kudumisha umoja wetu, kuwapa ushirikiano mzuri viongozi na wachezaji,” alisema Ahmed.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.