CHAMA NA KIBU WASITISHIWA MAZUNGUMZO SIMBA S.C


CHAMA NA KIBU WASITISHIWA MAZUNGUMZO SIMBA S.C


Kikosi cha Simba usiku wa juzi kilikuwa uwanjani visiwani  Zanzibar katika michuano ya Kombe la Ligi ya Muungano na kufanikiwa kufuzu kwenye fainali ya michuano hiyo kwa kuifunga KVZ mabao 2-0, lakini huku nyuma mabosi wa klabu hiyo wamefanya kitu kimoja kinachosthua dhidi ya mastaa wa timu hiyo, Clatous Chama, Kibu Denis na Saido Ntobazonkiza ambao mikataba yao ipo ukingoni.

Mabosi wa klabu hiyo wamedaiwa kusitisha mazungumzo waliyokuwa wameanza kufanya na wachezaji hao na wengine ambao mikataba yao inaelekea mwishoni na mustakabali wa wakali wengine wa kikosi hicho kinachoshika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara inayoongozwa na Yanga na kufuatiwa na Azam nafasi ya pili.

Uamuzi huo unaelezwa umekuja baada ya timu hiyo kuwa na matokeo mabaya yaliyosababisha presha kubwa ya nje ya uwanja na kuvuruga mipango na malengo mengi ya kikosi hicho kwa msimu huu ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kutolewa mapama katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) hivi karibuni.

Mwanaspoti linajua kabla ya hapo Simba ilikuwa imeanza mazugumzo ya kuongeza mikataba kwa baadhi ya nyota wao inayomalizika mwishoni mwa msimu huu sambamba na wengine waliotarajiwa kuboreshewa, lakini sasa imeacha kwa muda zoezi hilo kutokana na sababu mbalimbali.

Moja ya wachezaji waliokuwa kwenye mazungumzo ya kuongezewa mkataba kikosini hapo amethibitisha jambo hilo kusitiswa ghafla.

“Mazungumzo yalikuwepo, lakini ghafla wamesema zoezi la mikataba mipya limesitishwa hadi mwisho wa msimu. Kuna sababu nyingi zipo ukifuatilia utapata majibu ya kutosha kwani vitu vingi kwa sasa viko wazi,” alisema staa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Mwanaspoti halikuishia kwa nyota huyo, liliamua kuwatafuta baadhi ya viongozi wa Simba na wengi wao waliruka swali hilo na wengine kuomba kutotajwa baada ya kutoa ufafanuzi.

“Nikuhakikishie hadi sasa hakuna mchezaji hata mmoja ameongezewa mkataba na mazungumzo yamesitishwa kutokana na sababu kuu mbili hadi tatu. Moja, inasubiriwa ripoti ya kocha, pili hii presha imetuvuruga sana kuanzia viongozi hadi wachezaji wenyewe hivyo tunasubiri kwanza upepo huu upite,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo na kuongeza;

“Lakini, kuna panga kubwa litapita baada ya msimu kumalizika, hivyo tunataka yote hayo yafanyike kwa pamoja, sio unampa mkataba mpya mchezaji halafu ligi inapomalizika unakuwa haumhitaji na kutakiwa kumwondoa, hili hatulitaki.”

Chanzo kingine kiliwataja Chama, Kibu na Saido ni baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye mazungumzo ya kimkataba lakini yamesitishwa kutokana na uamuzi huo uliofikiwa na mabosi wa klabu hiyo waliochefukwa na matokeo ya kufungwa tena na watani wao Yanga katika Dabi ya Karikoo iliyopigwa wikiendi iliyopita.

Miongoni mwa wachezaji wa Simba wanaomaliza mkataba mwishoni mwa msimu huu ni John Bocco ambaye kwa sasa ni kama amejitenga na timu akiwa anafundisha kikosi cha vijana cha timu hiyo, pia wamo beki Shomari Kapombe, Luis Miquissone, Sadio Kanoute na Kennedy Juma.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya Simba zinaeleza, Simba ipo tayari kuwaongeza mikataba mipya Chama, Kibu, Kapombe, Kanoute na Kennedy Juma kama wataafikiana vyema, lakini imeahirisha jambo hilo baada ya kocha mkuu Abdelhack Benchikha kuwaeleza anataka wachezaji wapya atakaofanya nao kazi kwa msimu ujao.

Inaelezwa Benchikha anataka kujenga Simba mpya ambayo itakuwa na mabadiliko makubwa ya wachezaji na kiuchezaji, hivyo inaelezwa hiyo ni sababu kuu iliyofanya mazungumzo na mastaa hao kupigwa ‘stop’ kwa sasa bila kujali kama ni wale mikataba inaisha au wale waliokuwa wakitakiwa kuboreshewa mikataba.

Aidha kama hilo litafanikiwa, huenda Simba ikavunja benki kusajili majembe mapya atakayopendekeza Benchikha ambaye inaelezwa yupo tayari kuondoka kikosini hapo kama hatatimiziwa mahitaji yake ya usajili mwisho wa msimu huu.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alipoulizwa jana alisema kwa sasa timu imeweka nguvu zaidi kwenye mechi zijazo na baada ya msimu huu kuisha watarejea kwa kishindo.

“Kwa sasa tunaangalia zaidi kilicho mbele yetu, tuko katika kipindi cha mpito, nadhani mambo ya usajili na mengine ya namna hiyo tutayatolea taarifa pale muda wake utakapofika,” alisema Ahmed Ally.

Licha ya kuanza msimu kwa kutwaa Ngao ya Jamii, Simba imeshindwa kufika malengo ya kuvuka robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pia imetolewa Kombe la Shirikisho na sasa ipo hati hati kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kutokana kuachwa kwa watetezi, Yanga kwa alama zaidi ya 10.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad