Aliyekuwa kiungo mahiri wa klabu ya Yanga SC, Stephane Aziz Ki, ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Morocco katika klabu ya Wydad Casablanca, anaripotiwa kuwa katika hali isiyo ya kuridhisha ndani ya kikosi hicho. Taarifa zinaeleza kuwa kiungo huyo amekuwa akipitia kipindi kigumu baada ya kuonekana kupunguza kasi yake ya kawaida, kuongezeka kwa uzito na pia kupoteza mipira mingi uwanjani, jambo ambalo limeanza kuzua maswali kwa benchi la ufundi la timu hiyo.
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Morocco, hali hiyo imesababisha hofu kwa benchi la ufundi la Wydad na kuibua uwezekano wa kiungo huyo kuachwa katika msimu ujao. Inaelezwa kuwa iwapo hali haitabadilika, huenda akaachwa nje ya mipango ya timu hiyo hasa ikizingatiwa kuwa Wydad wako kwenye mazungumzo ya kumalizana na mchezaji mwingine, Lorch, anayesemekana kucheza kwa mkopo kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini. Endapo usajili huo utakamilika, nafasi ya Aziz Ki inaweza kuwa finyu zaidi.
Aziz Ki alihamia Wydad Casablanca kwa uhamisho wa bure kutoka Yanga SC, kufuatia makubaliano maalum yaliyofikiwa kati ya klabu hiyo ya Morocco, Yanga na meneja wake. Hii ina maana kuwa Yanga haikupokea fedha yoyote kutokana na uhamisho huo, jambo ambalo liliwashangaza mashabiki wengi wa soka Tanzania waliotarajia klabu ingepata faida kutokana na uwezo wa mchezaji huyo.
Kwa sasa, mashabiki na wachambuzi wa soka wanamfuatilia kwa karibu kiungo huyo ambaye aliwahi kuwa mhimili mkubwa wa kikosi cha Yanga. Katika kipindi chake akiwa Tanzania, alikuwa mmoja wa wachezaji waliotegemewa zaidi na mashabiki wa timu hiyo. Hata hivyo, mambo yanaonekana kubadilika kwa kasi tangu alipohamia nje ya Afrika Mashariki, na baadhi ya wachambuzi wanahoji kama mabadiliko ya mazingira na presha ya kucheza katika ligi ya Morocco imemshinda.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Yanga, mkataba wa Aziz Ki na Wydad ulikuwa na kipengele maalum ambapo miezi mitatu ya mwanzo walikuwa wanamwangalia kwa karibu kabla ya kufanya maamuzi ya kumpa mkataba wa kudumu wa miaka miwili. Ikiwa hataridhisha kiwango katika kipindi hicho, klabu hiyo inaweza kuamua kumtema.
Meneja wa Aziz Ki amesema kuna dalili kuwa mchezaji huyo huenda akatolewa katika kikosi msimu ujao, hasa kama usajili wa Lorch utakamilika. Ameeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa Aziz Ki kuondoka Morocco mapema zaidi ya matarajio ya wengi, lakini bado wanazo ofa kutoka vilabu mbalimbali vya Afrika Kusini ambavyo vinaonyesha nia ya kumsajili.
Hali hii imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Yanga, huku wengi wakielezea masikitiko yao kuona nyota wao wa zamani akikabiliwa na hali ngumu nje ya nchi, wakitamani kuona akirejea tena katika kiwango chake bora kama alivyokuwa Ligi Kuu ya Tanzania.