Leo saa 4:00 usiku, timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania 🇹🇿 Twiga Stars itashuka kwenye Uwanja wa Stade Municipal de Berkane, Morocco, kuivaa Mali 🇲🇱 katika mchezo wa kwanza wa Kundi C ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024.
.
Michuano hiyo ilianza rasmi jana kwa michezo ya kundi A, ambapo mwenyeji Morocco ilitoka sare ya mabao 2-2 na Zambia. Twiga Stars ni kati ya timu 12 zinazoshiriki fainali hizo za WAFCON na leo inaanza safari kwa kuminyana na Mali katika kundi gumu lililojumuisha pia watetezi Afrika Kusini na Ghana.
.
Licha ya kukosa huduma ya mshambuliaji nyota anayekipiga Brighton ya England, Aisha Masaka, aliyepata majeraha ya paja bado safu ya ushambuliaji ya Stars ina mastaa kama Clara Luvanga (Al Nassr), Opah Clement (atakosekana leo kutokana na kadi), Stumai Abdallah na kinda Jamila Rajabu (JKT Queens) wenye uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo.
.
Kwa mara ya mwisho timu zilipokutana katika WAFCON mwaka 2010, zikiwa pamoja na Afrika Kusini na Nigeria. Katika mchezo dhidi ya Mali, Stars ililala kwa mabao 3-2, mabao ya Mali yalifungwa na Aicha Konate, Diarra na N’Diaye ambao kwa sasa hawapo katika kikosi huku mabao ya Tanzania yakifungwa na Sophia Mwasikili, kwa sasa Meneja wa Simba Queens na Fatuma Swalehe.
.
Miaka imepita na sasa vikosi vyote viwili vimejaa na damu changa, huku Twiga Stars ikijivunia kikosi kipya chenye wachezaji wenye vipaji kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji.