Mchezaji Fei Toto Hakuna Kupoa Huko Ligi Kuu

 

Mchezaji Fei Toto Hakuna Kupoa Huko Ligi Kuu

Mchezaji Fei Toto Hakuna Kupoa Huko Ligi Kuu

Utamu wa Ligi Kuu Bara umesimama kwa muda wa kama wiki mbili ili kupisha michezo ya kimataifa. Taifa Stars inakabiliwa na mechi mbili mfululizo za kuwania fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026.

Stars itashuka uwanjani kuanzia Novemba 18 kuvaana na Niger kabla kumalizana na Morocco jijini Dar es Salaam Novemba 21, lakini ligi ikiwa imesimama kukiwa tayari zimeshapigwa jumla ya mechi 71 na mchezo mmoja ukiwa ni kiporo kinachozihusisha Mashujaa na Simba kukamilisha mechi za raundi ya tisa.

Ligi ya msimu huu ilianza Agosti 15 baada ya fainali ya mechi za Ngao ya Jamii zilizochezwa jijini Tanga na hadi kufikia Novemba 9, ilipochezwa mechi ya mwisho jumla mabao 161 yamezalishwa kwenye mechi hizo, huku Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiwa kwenye vita nzito na nyota wa kigeni.

Fei anawaongoza wazawa 62 waliofunga jumla ya mabao 92, akiwa ametupia matano, ikiwamo ‘hattrick’ dhidi ya Tabora United.

Katika mabao hayo 50 yaliyofungwa na wazawa, manne tu ndiyo yaliyofungwa kwa mikwaju ya penalti, ikiwa na maana 48 yametupiwa kawaida. Mabao hayo ya penalti kwa wazawa yamefungwa na Elias Maguri wa Geita, Danny Lyanga wa JKT Tanzania, Henock Mayala (Coastal Union) na Lucas Kikoti (Coastal Union).

Kwenye idadi hiyo ya mabao kwa upande wa wazawa mabao matatu kati ya hayo ni ya kujifunga yakitoka kwa Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Mohammed Makaka (Mtibwa Sugar) na Wilbol Maseke (KMC) dhidi ya Tanzania Prisons.

Kwa upande wa nyota wa kigeni ambao wapo zaidi ya 75 waliosajiliwa msimu huu miongoni mwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ni 31 wamefunga mabao 66 huku vinara wakiwa ni straika wa Simba, Jean Baleke, Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli wote Yanga wamepachika mabao saba kila mmoja kambani.

Katika mabao 66 ya wageni, saba yametokana na penalti likiwamo moja la Baleke. Penalti nyingine za wageni ni za Saido Ntibazonkiza, (Simba), Eric Okutu (Tabora United), Prince Dube (Azam FC), Obrey Chirwa (Kagera Sugar), Pacome Zouzoua (Yanga) na Fabrice Ngoy wa Namungo aliyekuwa wa kwanza msimu huu kufunga bao la penalti. Pia, wana mabao sita ya hat trick kutoka kwa Stephane Aziz Ki (Yanga) 3-2 dhidi Azam FC na Jean Baleke (Simba) 3-0 dhidi ya Coastal Union.

DR CONGO YAFUNIKA

Katika mabao 66, yaliyofungwa na mapro wa kigeni, DR Congo ndio iliyochangia mengi zaidi, ikifuatiwa na Zambia kisha Ivory Coast, Burkina Faso, Uganda na Ghana.

Kwa mujibu wa rekodi za mechi hizo tisa za Ligi Kuu, DR Congo pekee imezalisha jumla ya mabao 16, yakiwamo 14 ya Baleke na Maxi, moja moja ya Fabrice Ngoy na Fabrice Ngoma wa Simba.

Zambia imezalisha mabao manane, nyota wawili wa Simba, Moses Phiri amepachika matatu Clatous Chama akifunga mabao mawili, Keneddy Musonda mawili na lingine kutoka kwa straika wa Mzambia, Obrey Chirwa aliyefunga moja.

KI JESHI LA MTU MMOJA

Kiungo wa Yanga, Stephane Aziz KI kwa upande wake ameibeba Burkina Faso kwa kufunga mabao saba na kuifanya nchi hiyo kuingia kwenye orodha ya zilizozalisha mabao mengi.

PACOME, YAO

Nyota wawili wa Yanga, Pacome Zouzoua, Yao Kouassi wameibeba Ivory Coast kwa kufunga jumla ya mabao matano ikiwa ni nchi ya tatu iliyozalisha mabao mengi kwenye Ligi Kuu hadi sasa.

Pacome akifunga manne, huku beki la kazi, Yao akiwa na bao moja na kuifanya nchi ya Ivory Coast kuandika historia kwa sasa kwenye ligi ikichangia mabao mengi.

Mataifa yanayoifuata Ivory Coast ni Uganda na Ghana nyota wake wamezalisha mabao manne kila mmoja. Ben John anayekipiga Tabora United ndiye aliyeibeba Uganda kwa kufunga mabao mawili akifuatiwa na beki wa Kagera Sugar, Disan Galiwango aliyefunga moja sawa Hassan Mahamoud (Geita Gold) kwa upande wa Ghana, Eric Okutu wa Tabora United amepachika mabao mawili straika wa Yanga, Hafiz Konkoni na Christian Zigah (Dodoma Jiji) wakipachika bao moja moja.

SAIDO NA DUBE WAMO

Jumla ya mataifa manne yanafuata kwenye orodha ya nchi zilizozalisha mabao mengi kwenye ligi hiyo, huku Prince Dube wa Azam FC akiibeba Zimbabwe akiwa na mabao matatu huku kiungo wa Simba, Said Ntibanzonkiza akiibeba Burundi yenye maboa mawili, sawa na yaliyofungwa na nchi za Cameroon na Kenya. Cameroon imechangia mabao hayo kupitia winga wa Simba, Willy Onana na Moubakarak Amza wa Ihefu ambao kila mmoja amefunga bao moja kama ilivyo kwa Wakenya Elvis Rupia wa Singida Big Stars na Joshua Nyatini wa Tanzania Prisons.

SOMALIA, TOGO ZIMO

Katika orodha ya nchi zilizochangia mabao 39 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Senegal, Somalia na Togo nazo zimo, baada ya nyota wa nchi hizo nazo kufunga wakati ligi ikienda kusimama kwa muda. Marouf Tchakei, raia wa Togo anayekipiga Singida Big Stars amefunga mabao manne, Ibrahim Elias wa KMC kutoka Somalia na beki wa Azam FC, Cheikh Sidibe wa Senegal ni kati ya waliochangia mabao hayo kila mmoja akifunga bao moja na kufunga hesabu za mapro hadi sasa.

WAZAWA KAZI IPO

Japokuwa ni mapema mno kwa sasa kuanza kutabiri upepo utakavyokuwa hadi mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu, lakini ni wazi wazawa wanapaswa kukaza msuli kwani, nyota wa kigeni wapo moto kama msimu uliopita walipobeba Tuzo ya Mfungaji Bora.

Kwa sasa, Baleke, Azizi Ki na Maxi wanaongoza kwa mabao wakifuatiwa na Fei Toto mwenye mabao matano, kisha wageni wawili Pacome na Marouf Tchakei wenye mabao manne kila mmoja na mzawa, Matteo Antony wa Mtibwa Sugar, Habib Kyombo (SBS), Adam Adam (Mashujaa) wakifungana na Prince Dube, Moses Phiri kupachika mabao matatu kila mmoja.

Picha inaonyesha kasi ya ufungaji msimu huu katika mechi hizo 71 ni mdogo kulinganisha na mabao 161 ina maana ya wastani wake ni 2.26 tu ufungaji wa bao kwa kila mechi.

KADI

Wazawa wanaongoza kwa kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mizunguko tisa.

Abdallah Masoud ‘Cabaye’ (KMC), akiwa wa kwanza kupata kadi hiyo, Haji Ugando (Coastal Union) kwenye mchezo dhidi ya Simba, Abdulmalik Zakaria (Namungo) dhidi ya Kagera Sugar na Mwaita Gereza (Geita Gold) dhidi ya Dodoma Jiji.

Share this:

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.