Wakati mashindano ya soka ya kwa wachezaji wa ndani Afrika (CHAN), yakitarajiwa kuanza mwezi ujao, kuna maswali kibao nyuma yake. Hili ni tukio kubwa na muhimu kwa Tanzania 🇹🇿 si kwa sababu ya hadhi ya mashindano, bali kama sehemu ya maandalizi ya kuelekea AFCON mwakani, ambapo tunapaswa kuwa na kikosi cha ushindani na taifa lililo tayari kushindana katika medani za Afrika.
Hata hivyo, hali ilivyo sasa inatia shaka. Tumebakiwa na wiki chache kabla ya CHAN kuanza, lakini hatuonia dalili wala ishara ya maandalizi ya kueleweka. Hatuoni mikutano ya wadau, hatuoni mipango ya maandalizi wala ushirikishwaji wa jamii.
Viongozi wa soka nchini wako kimya kana kwamba hakuna mashindano yanayokaribia. Swali kubwa linabaki kuwa, je, kweli kuna CHAN wiki chache zijazo? Kama ipo kwa nini kuna ukimya mzito namna hii?
Zaidi ya TFF na mamlaka za soka, tunajiuliza pia mamlaka za kiserikali ziko wapi? Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iko wapi? Wizara ya Maliasili na Utalii? Mbona hatuoni juhudi za kuhamasisha wafanyabiashara, wawekezaji na jamii kwa ujumla kushiriki na kunufaika na mashindano haya?
Mashindano ya CHAN si kwa ajili ya TFF pekee. Ni fursa ya taifa kuonesha uwezo wa kuandaa mashindano makubwa, kukuza sekta ya michezo, na kwa namna ya kipekee kutangaza utalii na fursa za kiuchumi zilizopo nchini.
Tumeshuhudia nchi nyingine zikitumia mashindano haya kama jukwaa la kuimarisha uchumi wa wananchi wa kawaida kupitia biashara ndogondogo, huduma za hoteli, usafirishaji na burudani. Lakini hapa kwetu mpaka sasa hakuna shamrashamra mitaani, hakuna mabango wala matangazo yanayoonyesha ujio wa CHAN. Maeneo mengi ambayo yalipaswa kushirikishwa katika maandalizi haya hayajaonekana kuhamasika wala kufikiwa.
Tunajiuliza, utaratibu wa kuandaa jamii na kuifungua kiuchumi kupitia mashindano haya uko wapi? Je, kweli tumejipanga au tunasubiri wageni waje tupate aibu?
CHAN siyo tukio la kawaida ni dirisha la taifa letu katika medani ya soka Afrika, na tukishindwa kulitumia vyema mwaka huu tutakuwa tumepoteza nafasi ambayo hairudi kirahisi. Ni wakati wa mamlaka zote kuamka na kuonyesha dalili za maandalizi ya maana kabla hatujachelewa na kupoteza fursa