Dar es Salaam, Julai 8, 2025 – Hatimaye safari ya kiungo nyota wa Kimataifa kutoka Ivory Coast, Stephane Aziz Ki ndani ya Klabu ya Yanga SC, imefikia tamati rasmi baada ya kukamilika kwa uhamisho wake wa kudumu kwenda kwa miamba wa soka la Morocco, Wydad Casablanca.
Taarifa za ndani ya klabu ya Yanga SC zimethibitisha kuwa Wydad wametuma barua rasmi kwa uongozi wa Yanga mapema leo, wakieleza dhamira yao ya kuanzisha mchakato wa kumnunua Aziz Ki kwa mkataba wa moja kwa moja, kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya awali ya mkopo. Katika makubaliano hayo, kulikuwapo kipengele maalum kilichowapa Wydad fursa ya kumsajili kiungo huyo kabla ya tarehe 10 Julai 2025.
Baada ya mazungumzo ya kina na makubaliano baina ya pande zote mbili, Yanga wamekubali ombi hilo la Wydad, na sasa nyota huyo wa zamani wa ASEC Mimosas amejiunga rasmi na klabu hiyo ya Morocco kwa mkataba wa kudumu. Uhamisho huu umeifanya Yanga kuingiza zaidi ya Shilingi bilioni 1.7, kiasi ambacho ni kati ya makubwa zaidi kuwahi kupatikana na klabu hiyo kwa mchezaji mmoja.
Stephane Aziz Ki alijiunga na Yanga mwaka 2022 akitokea Ivory Coast na kwa muda wote aliokaa Jangwani, ameacha alama isiyofutika katika historia ya klabu hiyo. Alikuwa mhimili wa safu ya kiungo na sehemu muhimu ya mafanikio ya Yanga ndani na nje ya Tanzania, akiisaidia klabu hiyo kutwaa mataji ya Ligi Kuu ya NBC, Kombe la Shirikisho (ASFC), pamoja na kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka 2023.
Mbali na umahiri wake uwanjani, Aziz Ki pia alikua mchezaji mwenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa Yanga, akivutia maelfu ya wafuasi kupitia uwezo wake wa kupiga pasi za mwisho, kupiga mashuti ya mbali, na kusimamia mipira ya adhabu kwa ustadi mkubwa.
Kwa sasa, Aziz Ki ataendelea na maisha yake ya soka katika klabu ya Wydad Casablanca, moja ya timu kubwa na zenye historia ndefu katika soka la Afrika. Uhamisho huu unadhihirisha dhamira ya Wydad kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Kwa upande mwingine, Yanga SC wanasalia na jukumu la kuziba pengo lake, huku wakielekeza macho katika soko la usajili kusaka mbadala wake mwenye uwezo wa kuendelea kuleta tija katika safu ya kiungo.
Uongozi wa Yanga umethibitisha kuwa uhamisho huo umekamilika kwa mafanikio, huku wakiishukuru Wydad kwa ushirikiano wao na kumtakia Aziz Ki mafanikio katika hatua mpya ya maisha yake ya soka.