Yametimia, Yanga imemtangaza kocha raia wa Ujerumani Sead Ramovic kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyetupiwa virago.
Saa chache baada ya Yanga kutangaza kuachana na Gamondi,imemtangaza Mjerumani huyo ambaye alianza msimu na TS Galaxy ya Afrika Kusini ambayo haina matokeo mazuri msimu huu.
Ramovic alitua nchini juzi usiku kimyakimya kuja kumalizana na mabosi wa Yanga na kufichwa kwenye hoteli moja kubwa jijini Dar es Salaam.
Yanga imemtangaza kocha huyo kupitia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, lakini ikielezwa kuwa kesho msaidizi wake naye atatua nchini kuchukua nafasi ya Moussa Nd'ew ambaye aliondolewa pamoja na Gamondi.
Ramovic aliyezaliwa jiji la Stuttgart miaka 45, iliyopita hana tofauti sana na mtangulizi wake Gamondi kwa aina ya falsafa ya soka akipenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao timu hiyo inautumia.
Timu pekee aliyodumu kwa muda mrefu akiwa kocha ni TS Galaxy aliyoitumikia kwa takribani miaka mitatu kuanzia Oktoba Mosi 2021.
Hata hivyo, kocha huyo ambaye ni kipa wa zamani wa VfL Wolfsburg na Borussia Mönchengladbach ambazo ni moja ya klabu kubwa nchini Ujerumani atatakiwa kuwatuliza mashabiki wa Yanga kwa mafanikio kufuatia kukosa rekodi kubwa ya mafanikio ndani ya soka la Afrika.