Kiungo wa klabu ya Juventus, Paul Pogba ambaye alifungiwa kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka minne amepunguziwa adhabu hiyo mpaka miezi 18 baada ya kufanikiwa kukata rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo.
Pogba raia wa Ufaransa alikumbwa na adhabu hiyo baada ya kupimwa na kukutwa na kiwango cha juu cha homoni ya Dehydroepiandrosterone (DHEA) homoni ambayo huchochea uzalishaji wa testesterone mnamo Agosti mwaka jana.
Hii inamaanisha kwamba mshindi huyo wa kombe la Dunia 2018 na Ufaransa atakuwa huru kurejea uwanjani mwezi Machi 2025 hivyo anatarajiwa kuanza mazoezi na klabu yake ya Juventus mwezi Januari kwa ajili ya kuanza kusakata kabumbu kwa mara nyingine.