Kwanini Bocco Hayupo Uwanjani? Tumemfukuza, Amekubali Kirahisi

 

Kwanini Bocco Hayupo Uwanjani? Tumemfukuza, Amekubali Kirahisi

Milimuona Kevin Yondani akiwa na kitambaa cha unahodha wa timu yake Geita Gold. Ilikuwa siku chache zilizopita. Nikakimbilia katika mtandao wa Wikipedia kutazama umri wake. Msela Kevin yupo uwanjani mpaka leo. Nadhani hata msimu ujao atakuwepo uwanjani.


Jina? Kelvin Yondani. Tarehe ya kuzaliwa? Oktoba 9, 1984. Umri? Miaka 39. Bado Kelvin anadunda katika nafasi ngumu ya ulinzi wa kati. Akiwa katika umri huu amekumbana na kina Fiston Mayele, Prince Dube, Jean Baleke na wengineo.


Kwa mujibu wa mtandao huo huo wa Wikipedia inaonyesha kwamba John Bocco ambaye jina lake lipo katika usajili wa Simba msimu huu ana umri wa miaka 34. Amepitwa miaka mitano na Yondani.


Kwanini Bocco hayupo uwanjani? Kwa sasa nasikia anasomea ukocha huku akifundisha timu ya Simba chini ya umri wa miaka 17. Ni baada ya kumfukuza na kumwambia amezeeka katika soka letu. Ni kitu ambacho tumekuwa tukifanya mara nyingi baada ya kumchoka mchezaji.


Mchezaji mwenye roho ndogo huwa anakimbia akiambiwa hivi. Sana sana kama anacheza Simba au Yanga. Huwa anaukubali uzee, anavunjika moyo, kisaikolojia anajiona mzee kweli. Inatokea sana kwa wachezaji wazawa. Wachache ndio wanaweza kuwa wabishi. Ni kama inavyotokea kwa Kelvin.


Mpaka leo nina uhakika kwamba Bocco angeweza kwenda katika timu nyingine ya kawaida isiyo na presha. Angeweza kufunga walau mabao saba kwa msimu yangeitosha timu hiyo. Iwe Coastal Union au Namungo ama Tanzania Prisons. Angeweza kufanya hivyo.


Bocco angesimama mbele katika timu ambayo inamtegemea ambayo inaamini katika ustaa wake. Ambayo ina mashabiki wachache wanaomtegemea angeweza kurefusha urefu wa maisha yake ya soka mpaka kufikia miaka 40 kuliko kujidanganya kuwa kocha.


Tusiende katika mfano wa Cristiano Ronaldo kwa sababu kuna watu wanaamini kwamba ana matunzo mazuri kuliko wachezaji wetu vipi Meddie Kagere amefanyaje? Kelele zilipokuwa nyingi na Simba walipoona hawamhitaji hakujidanganya kuingia katika kazi ya ukocha.


Mtandao wa Wikipedia unaonyesha kwamba Kagere ana umri wa miaka 37. Yuko wapi? Alikwenda Singida Big Stars halafu sasa yupo Namungo. Bado anadunda na hayo mabao machache anayofunga yanaisaidia timu yake. Ana uzoefu pia wa kuisoma mechi na kuwaambia wenzake nini cha kufanya uwanjani.


Kwetu sisi wachezaji wetu inabidi wawe wabishi. Maisha ya mpira sio Simba na Yanga tu, wakati mwingine wachezaji wa aina ya Bocco wanahitajika kufanya hisani ya kuchezea timu nyingine na kutoa chochote kilichobakia katika miguu yao.


Hawafanyi hivyo kwa sababu ya njaa. Wanapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya kueneza uzoefu wao na pia kuzisaidia baadhi ya klabu ambazo hazina wachezaji wazoefu. Lakini hapo hapo mabao saba kwa msimu yaliyobaki katika miguu yao yanatosha sana kuzisogeza timu hizi hasa katika dunia ya kisasa ambayo wafungaji wazuri wametoweka.


Bocco angekuwa ameondoka katika soka letu kwa sababu ya majeraha ningeweza kuelewa, lakini kwa umri wake alipaswa kudunda uwanjani kama ilivyo kwa Yondani na Kagere. Tatizo lake ameingia katika mkumbo wa kukubali kwamba ameisha.


Juma Kaseja aliwahi kukataa hilo kwa muda mrefu mpaka alipochoka kweli. Alienda zake Kagera Sugar, akazurura zake KMC. Ilifika mahala aliitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa. Hivi ndivyo wachezaji wengine wanavyopaswa kuiga nyayo.


Tatizo kubwa lililopo kutoka kwa wachezaji wa timu kubwa ni ukweli wanahisi timu ndogo zina njaa. Wanahisi kwamba itawasumbua zaidi kuishi katika maisha ya kukaa njiani kwa muda mrefu katika mabasi wakati wao walishazoea kupanda ndege hata katika safari fupi kama ya Dar es salaam kwenda Dodoma.


Wachezaji wetu wa timu kubwa wameshazoea kukaa katika kambi za kisasa na hoteli za kisasa na labda ndio maana wanasikia uvivu kwenda kumalizia maisha yao ya soka katika timu ndogo.


Haishangazi kuona kina Bocco wanakwepa kumalizia maisha huko.


Kinachofanyika kwa mchezaji aliyecheza muda mrefu katika klabu kubwa ni kwenda kuchukua kozi fupi ya ukocha na kisha kupewa ukocha msaidizi au umeneja. Baada ya hapo anaendelea kupanda ndege huku kazi yake kubwa ni kukusanya na kupanga jezi za wachezaji ambao hawamzidi hata kiwango kama akiamua kurudi uwanjani. Bocco anawezaje ghafla kuwa mfanyakazi wa Pa Jobe na kwenda kumgongea mlango wa chumba chake akimkumbusha muda wa mazoezi?


Tuongeze uchumi wa hizi timu za kawaida. Labda itawafanya baadhi ya wachezaji wakongwe kuangukia katika timu hizi na kisha kucheza kidogo. Kina Nsajigwa Shadrack wote walikubali kirahisi kwamba wamezeeka wakaacha mpira wakati wakiwa na nguvu za kucheza katika timu za kawaida. Ulaya kuna mfumo wa kuhama ligi kama Lionel Messi na Ronaldo walivyoamua kwenda katika nchi ambazo hazipo imara sana kiushindani wa soka lakini zina pesa. Ni kweli waliamua kutafuta machimbo ambayo mpira unaweza kukidhi mahitaji ya miili yao lakini pesa zipo. Sisi hatuna majirani wanaoweza kutusaidia katika hilo.


Lakini tunaweza kufanya kama vile ambavyo kina Rio Ferdinand, Sol Campbell na wengineo walifanya. Walihamia katika timu za kawaida na kutoa msaada walau kwa msimu mmoja au miwili kabla ya kuamua kutundika daluga moja kwa moja.


Hauwezi kuniambia kwamba Bocco anashindwa kuifungia Coastal Union mabao. Kwa ligi gani hasa ambayo imemfanya Bocco kujistaafisha kimya kimya na kuwa kocha wa kudumu wa kikosi cha vijana wa Simba huku akiwa hana majeraha?

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.