Simba imtimue anayesajili wachezaji

Simba imtimue anayesajili wachezaji


Tumeona wenyewe. Simba imekufa bao 1-0 mbele ya Al Ahly katika Uwanja wa Benjamin Mkapa hapo juzi. Ni historia mpya. Ni mara ya kwanza Al Ahly anashinda dhidi ya Simba hapa nchini.


Ilishakuja mwaka 1985 katika mechi za Kombe la Washindi Afrika (michuano iliyokuja kuunganishwa na ile ya Kombe la CAF mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika) Waarabu walikula 2-1 CCM Kirumba.


Mwaka 2019 na 2021 walikuja tena katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa na kunyuka bao 1-0 kila mechi na Oktoba tu mwaka jana Al Ahly ilikuja kucheza na Simba katika mechi ya robo fainali ya michuano mipya ya African Football League ngoma ikaisha kwa sare ya mabao 2-2.


Lakini juzi usiku ikitawala kila kitu uwanjani, Simba ilionekana timu ya kawaida sana mbele ya Al Ahly na kufungwa bao la mapema lililotokana na presha ya mabeki na kuwapa ushindi Waarabu Kwa Mkapa.


Hata hivyo, wala haishtui sana. Simba wana timu ya kawaida sana msimu huu. Yawezekana ndio timu yenye ushindani mdogo kuliko nyingine walizokuwa nazo miaka hii ya karibuni.


Wachezaji wengi wamechoka. Wachezaji wengi ni wazee. Wachezaji waliosajiliwa msimu huu wameshindwa kabisa kuonyesha utofauti.


Hebu fikiria kuhusu nyota waliotua dirisha dogo. Ni Babacar Sarr pekee aliyeanza katika kikosi cha kwanza. Wengine wako wapi? Wanajua wenyewe.


Huu ndio ukweli mchungu unaotakiwa kusemwa. Watu wanaofanya usajili pale Simba wanamrudisha nyuma mwekezaji, Mohammed 'Mo' Dewji. Wanamrudisha nyuma Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye siku hizi anaibeba Simba katika mabega yake.


Kuna mahali Simba haifanyi utafiti wake vizuri katika kubaini wachezaji mahiri na kuwasajili. Yawezekana inachukua nyota wenye majina makubwa lakini ambao hawaendani na falsafa ya timu.


Mfano msimu huu wachezaji wengi wamekuja na kushindwa kuleta utofauti. Ni Che Malone Fondoh na Ayoub Lakred ambao wameonyesha utofauti hasa katika mechi za kimataifa. Wengine kimewakuta nini?


Siwezi kuwalaumu sana kuhusu Luis Miquissone. Walimuuza kwenda Al Ahly akiwa mchezaji mahiri. Ni miaka miwili tu mbele waliona nafasi ya kumrudisha na wakafanya hivyo.


Ni kweli Miquissone alikuwa hachezi huko, lakini kwa akili ya kawaida ilikuwa ngumu kuamini kama atakuwa ameshuka sana. Tulidhani angehitaji miezi michache kuwa sawa na kurejea katika ubora wake, lakini bahati mbaya ameshindwa.


Ila hawa kina Omary Jobe na Fredy Michael sidhani kama wanafikia ubora wa aina ya washambuliaji ambao wanaweza kuibeba Simba katika mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni washambuliaji wazuri, lakini sio kwa daraja la Simba. Sio kwa malengo ya kule ambako Simba inataka kwenda.


Wachezaji wazawa ndio wameshindwa kabisa. Mfano yule David Kameta 'Duchu' alisajiliwa kuja kufanya nini? Ameshindwa kabisa kuwapa changamoto Shomari Kapombe na Israel Mwenda. Ameshindwa hata kuwa msaada kule kwa Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’.


Yule Abdallah Hamis bado hajaweza kuingia kwenye mfumo wa Simba. Bado Mzamiru Yassin anacheza vizuri kuliko yeye. Ndio sababu mechi ilivyokuwa ngumu kwa Sarr juzi, Abdelhak Benchikha alimtoa na kumuingiza Mzamiru.


Hawa kina Ladack Chasambi na Edwin Balua labda tuwape muda. Ni vijana wadogo pengine huko mbeleni wanaweza kuingia kwenye mfumo wa Simba. Hatuwezi kuwapa majukumu ya CAF kwa sasa. Ni watoto.


Ukitazama mechi ya juzi dhidi ya Al Ahly, Simba ilikosa straika mahiri tu wa kuamua mechi. Inakosa mastraika wa daraja la kina Meddie Kagere. Bahati mbaya wachezaji wanaocheza pembeni hawana lile daraja la Emmanuel Okwi au Miquissone kabla hajaenda kumaliza soka lake Uarabuni.


Kibu Denis anacheza vizuri. Ni mpambanaji, lakini sio mfungaji mzuri. Ndio maana tangu kuanza kwa msimu huu licha ya sifa zote, amefunga bao moja tu. Ingekuwa enzi za Okwi angekuwa na mabao hata 10.


Wachezaji wa safu ya kiungo nao wamekosa ule ubora wao wa kufunga. Ndio sababu Chama ana bao moja tu kwenye Ligi ya Mabingwa hadi sasa. Enzi zile angekuwa na mabao hata manne.


Ukweli ni kwamba Simba inatakiwa kufanya usajili mzuri kwenye dirisha kubwa. Mbona Yanga wameweza kwenye miaka hii miwili. Wamesajili wachezaji mahiri. Hawa kina Pacome, Maxi Nzengeli, Yao Kouassi wamesajiliwa msimu huu. Kwani Simba ilikuwa haiwaoni?


Yawezekana hawakuonwa na Simba. Kwanini? Kwa sababu watu wanaotafuta wachezaji pale Simba hawana macho mazuri ya kuona nyota mahiri. Wanabahatisha tu. Ndio maana wanakuja wachezaji watano, halafu mmoja ama wawili tu ndio wanaonekana wazuri.


Kwa mwenendo huu bado Simba itaendelea kusubiri kwa miaka kadhaa kufikia malengo yake ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Haijalishi kama Yanga itatolewa na Mamelodi Sundowns kwa mwaka huu, lakini kwa aina ya timu wanayojenga huenda wakafika nusu fainali kabla ya Simba.


Yanga wamejiimarisha katika eneo la usajili. Waliwahi kupigwa huko nyuma kwa kina Michael Sarpong, Yipke, Gael Bigirimana na wengineo. Kwa sasa hawataki kurudia makosa. Ndio maana kwenye usajili wa mwaka huu aliyefeli moja kwa moja ni Hafiz Konkon pekee.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.