Yondani: Tatizo Simba ileile

Yondani: Tatizo Simba ileile


Kipigo cha bao 1-0 ilichokipata Simba na kuitibulia rekodi ya nyumbani dhidi ya Al Ahly katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kimemuibua nahodha wa zamani wa timu hiyo, Yanga na Taifa Stars, Kelvin Yondani akisema tatizo la Simba haijabadilika kiuchezaji.


Yondani alisema licha ya kipigo hicho ilichopata juzi usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini anaamini timu hiyo ina nafasi ya kwenda kulipa kisasi ugenini iwapo tu itaamua kubadilika kiuchezaji, kwani imekuwa ikicheza vilevile kwa misimu mitano ya kufika hatua ya robo fainali za CAF.


Akizungumza na Mwanaspoti, Yondani alisema Simba ni msimu wa nne kucheza robo fainali katika Ligi ya Mabingwa na misimu mmoja ilicheza hatua hiyo kwa Kombe la Shirikisho na mara zote kung’olewa hatua hiyo kwa vile wachezaji hawabadiliki na hupambana kama wahapo kwenye mechi za mtoano.


Yondani alisema Simba inacheza huku ikiwa haiwaheshimu wapinzani na kuamini ikiwa nyumbani huwa haifungwi na matokeo yake imejikuta ikiwasononesha mashabiki na kung’oka hatua hii mara zote ilizocheza.


“Kwa upande wa benchi la ufundi mpango ulikuwa vizuri, lakini wachezaji ndio walishindwa kufanya kazi kwa usahihi ili kuipa timu matokeo mazuri uwanja wa nyumbani. Kucheza mechi za mtoano zinahitaji hesabu kali, Al Ahly ikiwa hatua hizi hujitofautisha kabisa na ile ya makundi,” alisema Yondani.


“Hizo ni changamoto ambazo Simba imekuwa ikikutana nazo mara nyingi, lakini bado wanazingatia kiwango badala ya hesabu za ushindi. Jana ilicheza vizuri, lakini Al Ahly iliondoka na ushindi ugenini. Naamini timu ina nafasi ya kujisahihisha, lakini lazima ibadilike kiuchezaji mtoano haitaki shoo shoo.” Yondani alisema Simba ina nafasi ya kufanya vizuri ugenini kama mipango itasukwa vyema na kusahau matokeo iliyopata nyumbani.


“Kwanza wakiwa ugenini wanatakiwa kuwa makini dakika 20 hadi 25 za kwanza wasiruhusu bao watampa wakati mgumu mpinzani kuhakikisha anaufanya mchezo uwe wa ushindani tofauti na ilivyokuwa mchezo wa nyumbani,” alisema.


Beki huyo aliyeitumikia Simba kwa misimu sita kati ya 2006-2012 kisha akahamia Yanga aliyoitumikia hadi 2020 kwa sasa yupo katika kikosi cha Geita Gold baada ya awali kupita Polisi Tanzania.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.