Simba kufanya uamuzi mgumu

Simba kufanya uamuzi mgumu


Simba inakuna kichwa jinsi ya kupindua meza baada ya kichapo cha bao 1-0 ilichopata kutoka kwa Al Ahly ya Misri katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku vigogo vya klabu hiyo wakijipanga kufanya uamuzi mgumu wa kufumua kikosi kizima walichonacho.


Mabosi wa Simba wamebaini kuwa kikosi kilichopo kinahitaji mabadiliko makubwa ili kufanikisha ndoto za kuiona ikifika anga za mbali katika michuano ya kimataifa na hata hapa nyumbani kulinganisha na hali waliyonayo kwa sasa.


Simba katika dirisha dogo iliingiza wachezaji watatu wa kigeni akiwamo kiungo mkabaji Babacar Sarr na washambuliaji Fredy Michael na Pa Omari Jobe mbali na viungo washambuliaji wazawa Ladack Chasambi, Saleh Kalabaka na Edwin Balua ambao wameshindwa kufanya maajabu kikosini.


Fredy na Pa Jobe walisajiliwa kuchukua nafasi za Jean Baleke na Moses Phiri ambao kwa pamoja waliifungia timu hiyo mabao 11 katika Ligi Kuu Bara, mbali na mabao mengine ya CAF, lakini wachezaji hao wameshindwa kuonyesha uwezo na kuwazindua mabosi wa Msimbazi.


Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Issa Masoud amesema wana kila sababu ya kufanya usajili mkubwa dirisha lijalo ili kutorudia makosa yanayojitokeza mara kwa mara na kuigharimu timu.


Masoud aliyasema hayo muda mfupi baada ya Simba kupoteza mchezo wa kwanza wa robo fainali Ligi ya Mabingwa mbele ya Al Ahly iliyowafunga bao 1-0 na kuwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Misri kupata ushindi dhidi ya Mnyama ikiwa ardhi ya Tanzania.


Kigogo huyo alisema pamoja na kipigo hicho, mashabiki hawatakiwi kuvunjika mioyo, japo wanatambua wameumia kwa matokeo, lakini hata wao kama viongozi wameumia zaidi kwa sababu wanafanya juhudi kubwa kuwekeza ili kupata mafanikio ila mambo yanakuwa magumu.


“Soka ni mchezo wa hisia kila mtu unamuumiza, lakini sisi kama viongozi tunaumia sana kwa sababu tunafanya vitu vingi ambavyo vinaonekana na visivyoonekana kwa ajili ya kuhakikisha tunapata matokeo mwisho wa siku havitokei tutafanya marekebisho dirisha kubwa la usajili,” alisema Masoud.


“Matokeo yasiyo ya kutarajiwa ambayo yamekuwa yakitoa hisia mbaya kwetu kutokana na kuumizwa nayo yanatupa sababu ya kurudi sokoni kufanya usajili mkubwa ili kujenga timu bora na ya ushindani.” Akizungumzia mchezo kwa ujumla alisema ulikuwa upande wa Simba, lakini walishindwa kutumia nafasi nyingi walizotengeneza wakiamini bado wana nafasi ya kwenda kupata matokeo mazuri ugenini kutokana na uwepo wa kocha Abdelhak Benchikha ambaye ni mzoefu wa michuano hiyo.


“Ni kweli tumepoteza mechi, lakini tumepoteza mchezo uliokuwa ni wetu kwa sababu ukifanya utafiti wa huu mchezo utagundua tumefanya mashambulizi mengi kuliko wapinzani, lakini mpango wa kocha haukuwa mzuri kwa kuanza bila mshambuliaji halisi,” alisema Masoud.


Aliongeza kuwa sababu ya kupoteza mchezo ni kutokana na ugumu walioupata kutoka kwa mpinzani akifunga njia za wachezaji kushambulia licha ya kupata nafasi na kushindwa kuzitumia.


“Mchezo ulikuwa mgumu kwetu kutokana kukutana na timu ambayo ilikuja na mbinu ya kujilinda zaidi na kufunga njia za wachezaji kama Clatous Chama kushindwa kupata uwazi wa kupenya licha ya nafasi nyingi walizozipata kushindwa kuzitumia,” alisema Masoud na kuongeza:


“Haikuwa bahati yetu licha ya kuwa uwanja wa nyumbani tunajipanga tukimtumia zaidi kocha Benchikha ambaye ni mzoefu na bora kwenye mbinu atatupa mchezo mzuri na wa ushindani ambao utatupa nafasi ya kusonga hatua inayofuata.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad