Kutokuwa na wachezaji wake nyota, ilikuwa sababu ya Yanga kushindwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns uliopigwa jana usiku.
Yanga ikicheza kwa mbinu za hali ya juu ilitoka suluhu na Mamelodi kwenye mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Mkapa, siku moja baada ya Simba kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye hatua hiyo. Marudio ya mechi zote ni wikiendi ijayo.
Kipindi cha kwanza mchezo huo ulianza taratibu, huku Mamelodi ikionekana kucheza kwa kujilinda zaidi sawa na ilivyofanya Yanga.
Siku moja kabla ya mchezo huu kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema ana wachezaji ambao wanasumbuliwa na majeraha na hawezi kuwatumia kwenye mchezo huu.
Kikosi cha Yanga cha jana kilianza bila mastaa watatu wakubwa Pacome Zouazoa, Khalid Aucho na Yao Kouassi ambao wamekuwa wachezaji tegemeo kwenye timu hiyo katika michezo ya kimataifa na ni miongoni mwa sababu iliyochangia kutopata ushindi.
Licha ya nafasi ya Aucho kuzibwa na Mkude, Pacome ilizibwa na Clement Mzize na ya Yao ilichezwa na Maxi Nzengeli.
Kutokana na kutokuwepo kwa Pacome ambaye ana mabao matatu na asisti moja kwenye mashindano hayo katika hatua ya makundi, kutokuwepo kwake kunaweza kuwa sababu ya kuifanya timu kushindwa kupata matokeo.
Kwa kawaida Pacome hucheza na Aziz Ki pamoja na Nzengeli katika eneo la ushambuliaji, na kutokuwepo kwake na wenzake kulimlazimu Gamondi kubadili mfumo ili kuziba nafasi zao.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza Jonas Mkude alianzia kwenye mchezo huu, ambapo alionyesha kiwango kizuri.
Tofauti na namna ambavyo Yanga imezoeleka kucheza kwa mfumo wa 4-3-3 au 4-2-3-1, Gamondi aliamua kubadilika na kuibuka na mfumo wa 5-3-2 kwa kuanza na mabeki watatu wa kati ambao ni Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca'.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Yanga ilianza dakika 45 za kipindi cha kwanza kwa kasi, huku ikipoteza nafasi ya wazi kupitia kwa Clement Mzize ambaye shuti lake liliishia mikononi mwa kipa wa Mamelodi Sundowns, Ronwen Williams.
Uwepo wa Aziz KI na Mudathir Yahya kwenye eneo la kiungo huku Miguel Gamondi akianza na washambuliaji wawili Kennedy Musonda na Mzize kulionekana kuwachanganya Mamelodi ambao muda mwingi walikaa kwenye lango lao.
Sababu nyingine iliyoifanya Yanga ishindwe kuibuka na ushindi ni Mudathir na Aziz Ki kufanya kazi ya kukaba zaidi badala ya kupeleka mashambulizi mbele kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwenye michezo mingine pia Maxi Nzengeli naye alijikuta akifanya kazi kubwa katikati kuliko kwenda mbele kuongoza mashabulizi.
Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Yanga ilikuwa bora kwa kupiga mashuti matano huku matatu yakilenga lango, Mamelodi wenyewe walipiga mashuti matatu huku moja ndio likilenga lango.
Sub ya Aziz KI
Mchezaji aliyekuwa akiisumbua sana Mamelodi Sundowns Stephen Aziz Ki, aliumia na kutoka nje dakika ya 74, hali ambayo iliwapa pia Mamelodi nafasi nzuri ya kutawala kwenye eneo la katikati ya uwanja, ambapo alitoka pamoja na Kennedy Musonda na kuingia Augustine Okrah na Joseph Guede ambao hawakuwa na makali zaidi.
MKUDE FRESHI
Pamoja na kwamba hakuwa akipewa nafasi na wengi kuwa ataanza kwenye mchezo huo wa robo fainali, Jonas Mkude ameonyesha ukomavu wake.
Mkude aliifanya Yanga kuwa na utulivu na kuwa imara kwenye eneo hilo la kati ambalo amezoeleka kucheza Khalid Aucho ambaye alikuwa akiuguza majeraha.
Kiungo huyo wa zamani wa Simba, hakuonekana mwenye papara, mara nyingi pasi zake zilionekana kuwafikia walengwa huku akirahisisha mashambulizi kwa uwezo wake wa kupiga pasi ndefu katika maeneo ya pembeni