Wabunge wasafirisha miili waliopoteza maisha ajalini

Wabunge wasafirisha miili waliopoteza maisha ajalini

Klabu ya Simba kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge wameshirikiana kusafirisha miili ya mashabiki wawili wa timu hiyo waliopoteza maisha wakienda Dar es Salaam kuangalia mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya timu hiyo na Al Ahly ya Misri uliopigwa jana.


Mashabiki wawili wa Simba walipoteza maisha katika ajali ya basi dogo iliyotokea Machi 29, mwaka huu katika eneo la Vigwaza mkoani Pwani, ambapo klabu hiyo na baadhi ya wabunge wametoa fedha ikiwa ni rambirambi pamoja na gharama za matibabu kwa majeruhi.


Miili ya mashabiki waliofariki dunia imesafirishwa kwenda Mbeya kwa ajili ya mazishi, huku majeruhi 12 kati ya 17 wakiruhusiwa kutoka hospitali na Simba imegharimia safari ya kuwarudisha kwao, Mbeya.


Spika wa Bunge ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ametoa Sh2 milioni na gharama za majeneza yaliyotumika kuwasafirishia marehemu.


Dk Tulia ametoa fedha hizo baada ya kuwatembelea majeruhi wa ajali hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze akiambatana na mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete.


Wengine waliotoa rambirambi ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa aliyetoa Sh1 milioni, ilhali Ridhiwani akilipia gharama zote za matibabu kwa majeruhi ambazo ni Sh3.5 milioni.


Naye mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda ametoa Sh500,000 na huduma ya chakula kwa majeruhi, huku mbunge wa Rungwe, Antony Mwantona akitoa rambirambi ya Sh500,000.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.