Benchikha hatoboi Simba, yeye sio CEO wala Mwenyekiti - Shabiki

Benchikha hatoboi Simba, yeye sio CEO wala Mwenyekiti - Shabiki


Shabiki kindakindaki wa Klabu ya Simba, Mjata Mjata anasema kuwa kama tatizo la Simba lilikuwa ni kwenye benchi la ufundi, basi kupitia Kocha Mpya Benchikha Simba wamepata suluhisho, lakini kama tatizo lilikuwa ni ndani ya Uongozi wa Simba basi Benchikha hawezi kutoboa.


Mjata amesema kuwa, matatizo ya Simba sio tu kwenye benchi la ufundi lakini pia yanachangiwa na viongozi wa ngazi za juu wa klabu hiyo ambao amedai kuwa kwa asilimia kubwa inaonekana hawa maelewano kati ya wao kwa wao.


“Kama matatizo yanayoendelea kwenye Klabu ya Simba yanahusisha tu masuala ya kiufundi, basi tumepata dawa kwa sababu Benchikha ni kocha mzuri. Lakini kama matatizo hayo ni zaidi ya benchi la ufundi kwa maana ya kwamba yanahusisha uongozi, Benchikha hawezi kutoboa kwa sababu yeye sio CEO wa Simba, sio Mwenyekiti wala Simba wala Mwekezaji wa Simba, Benchikha ni kocha wa Simba.


“Tumempata kocha mkubwa ambaye amekuja kwenye Klabu ya Simba, Benchikha anaweza akatusaidia kwa asilimia 50 na asilimia 50 asitusaidie. Kwenye masuala ya kiufundi hakuna shida yoyote kwa sababu ni kocha mkubwa.


“Ninavyojua mimi baadhi ya matatizo ya Simba yako ndani ya uongozi wa Timu. Kwa hiyo kama tunataka kufanya vizuri, viongozi waliopo madarakani wamalize tofauti zao ili Benchikha na benchi lake la ufundi wafanye kazi vizuri.


“Juzi hapa (baada ya mechi ya ASEC Mimosas) vilifanyika vikao vingi sana, Kocha Selemani Matola alisema baada ya wachezaji kuzungumza na viongozi, wachezaji walifanya mazoezi bora na intensity ya hali ya juu ambayo hata yeye mwenyewe hajawahi kuyashuhudia akiwa Simba.


“Maana yake kulikuwa na vitu ndani, viongozi wakawafuata wachezaji wakazungumza nao, walipomaliza kikao mazoezi yakafanyika kwa nguvu, kwa hiyo tatizo sio wachezaji tu hata viongozi walikuwa wamechangia,” amesema Mjata Mjata.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.