Aliyemteua Eng. Hersi ni Motsepe

 

Aliyemteua Eng. Hersi ni Motsepe

Wiki iliyopita kuna jambo liliripotiwa vibaya na baadhi ya vyombo vya habari (sio Mwanaspoti wala Mwananchi) na pia wachambuzi baadhi.


Jambo lenyewe lilikuwa ni uteuzi wa Injinia Hersi Said wa kuwa Mjumbe wa Kamati za Maandalizi za Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) na Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN).


Baadhi ya vyombo vya habari na wachambuzi wakaripoti kwamba uteuzi wa Injinia Hersi umefanywa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia kwa vile ndiye aliyetangaza hilo wakati wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika Iringa.


Kiuhalisia walioripoti hivyo hawakututendea haki wapokeaji, hawamkumtendea haki Rais Karia wala Rais Motsepe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika kwa sababu hawakuripoti kitu sahihi na hapo kuna mambo mawili inawezekana yamesababisha hilo kutokea.


Jambo la kwanza ni kutokuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kushindwa kuripoti sahihi maana Karia katika hotuba yake alisema wazi kuwa anampongeza Hersi na wengine walioteuliwa na CAF sasa iweje aliyewapongeza wenzake kwa kuteuliwa na yeye akiwa miongoni mwa wateuliwa naye ndio mteuaji?


Lakini jambo la pili ni kutokuwa na ufahamu na uelewa wa namna CAF inavyoendeshwa na katiba yake ambapo kwa anayefahamu hivyo asingeweza kuripoti kitu kama hicho.


Kwa mujibu wa katiba ya CAF, mwenye mamlaka ya uteuzi wa kamati au mjumbe wa kamati yoyote iliyo chini ya shirikisho hilo ni Rais wa CAF na uteuzi huo unapitishwa na kamati ya utendaji baada ya shirikisho au chama cha nchi husika kuridhia uteuzi huo.


Hivi sasa Karia anaingia katika Kamati ya Utendaji ya CAF kwa kofia ya kuwa Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kama ilivyo kwa marais au wenyeviti wa kanda nyingine za soka barani Afrika.


Katiba ya CAF haijampa mamlaka ya kuteua kwa vile yeye ni mjumbe kama ilivyo kwa wengine hivyo kusema kuwa ndiye amefanya uteuzi wa Injinia Hersi sio sahihi na walioripoti hivyo pengine walitakiwa kujipa muda kidogo wa kujiridhisha kabla hawajatupatia habari hiyo.


Alichokifanya Karia ni kuthibitisha tu na kuutangaza uteuzi wa Injinia Hersi uliofanywa na Motsepe na sio yeye ndio kateua

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.