YANGA Mabingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo, inaripotiwa wataweka kambi ya maandalizi Rwanda wiki chache zijazo. Lakini habari mpya ni jina la kocha kijana Mfaransa mwenye uzoefu na soka la Afrika limetua mezani kwao.
Kocha huyo ni Romain Folz (35), lakini sifa yake kubwa ikitajwa ni soka la kushambulia lenye pasi nyingi na mtu makini kazini. Kazi yake ya mwisho ilikuwa Msaidizi kwenye benchi la Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mwaka jana.
Habari ambazo nimezipata ni Yanga wako kwenye mazungumzo na kocha huyo miongoni mwa tageti zao kuchukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyetimkia Ismailia ya Misri. Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika; “Makubaliano na Kocha Romain Folz kujiunga na Yanga yako karibu kukamilika. Kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu mkataba wa miaka miwili pamoja na chaguo la mwaka mmoja wa ziada. Kulikuwa na makocha wengine waliokuwa wanatazamwa, lakini klabu imeonyesha nia kubwa kwa Kocha Folz.”
Folz amejijengea jina Barani Afrika baada ya kuifundisha Township Rollers ya Botswana, alihamia Afrika Kusini mwaka 2022 kujiunga na Marumo Gallants na alikuwa kocha mdogo zaidi katika Ligi Kuu wakati huo. Baadaye alihamia AmaZulu FC, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo mwaka 2023.
Katika msimu wa 2024/25, alijiunga na Mamelodi Sundowns kama kocha msaidizi lakini aliacha kazi pamoja na kocha mkuu Manqoba Mngqithi, miezi michache baada ya msimu kuanza.