Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema wala hashangazwi na kiwango alichoonyesha kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua kwani alishawahi kuwaambia mabosi wake wa zamani kwamba kikosi hicho kinahitaji staa kama huyo, huku akishauri kuhusu usajili ujao.
Robertinho ambaye alitua Simba Januari 3, 2023, aliondoka Novemba 9, 2023 siku chache baada ya kuchezea kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Robertinho alisema alichofanya Pacome msimu wa 2024/25 hakijamshangaza kabisa kwa sababu alishamuona tangu msimu wake wa kwanza alipofika.
Alisema kuwa alishawahi kuwaaambia mabosi wa timu hiyo kwamba ili Simba irudi kwenye makali yake inahitaji kiungo jasiri na mwenye kasi kama raia huyo wa Ivory Coast.
“Pacome akiwa na mpira ukiwa kocha wa timu pinzani unakuwa na presha mbili, kuomba akosee hesabu zake au wachezaji wako waongezeke kupambana naye kwa nguvu na wafanikiwe kumtibulia hesabu,” alisema kocha huyo raia wa Brazil.
Pacome katika msimu uliomalizika hivi karibuni, alionyesha kiwango kizuri kilichowavutia wengi na kumtaja kwamba ndiye anastahili kuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu Bara ambapo alifunga mabao 12 na asisti tisa akiisaidia Yanga kubeba mataji matano ambayo ni Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).
Robertinho ametoa ushauri wa wachezaji wanaopaswa kusajili ili kuirudisha timu hiyo kwenye ushindani wa mataji.
“Kama Simba ikiendelea kuchukua wachezaji wa kawaida itakuwa ngumu kupindua ufalme wa Yanga. Kwenye kuchukua mataji kitu kinachoniumiza bado mashabiki wa Simba wanakosa raha mbele ya Yanga.