Faida ambayo Azam wanakwenda kupata kwa Ibenge ni kuwa watakuwa katika nafasi nzuri ya kupata mastaa wengi wazuri kutoka DR Congo. Anawafahamu mastaa wengi wazuri kutoka huko na katika siku za karibuni inaonekana soko lake DR Congo huwa linatuletea wachezaji wazuri kuliko kutoka katika mataifa mengine. Labda kwa sasa wanashindana na Ivory Coast.
Faida nyingine ambayo Azam wanakwenda kuipata kwa Ibenge ni kwamba anaufahamu vyema mpira wa Afrika ndani na nje ya uwanja. Wakati mwingine ni bora kumchukua kocha kama Ibenge kuliko kuleta kocha bora kutoka Ufaransa au Ujerumani ambaye hafahamu vyema misingi ya soka la Afrika, siasa za mpira ndani na nje ya uwanja.
Na sasa tunamsubiri Ibenge kuona namna ambavyo ataitengeneza Azam. Haitakuwa kazi rahisi sana. Kuna sehemu mbili ambazo tunasubiri kwa hamu kuona akiisuka Azam. Kuwa nzuri ndani ya ligi yetu na katika michuano ya kimataifa.
Akitufanyia mambo ya Pyramids tutaamini kweli Azam huwa inakwama katika soka la ndani kwa sababu ya fitina za hapa na pale.
Nisisahau pia kuipongeza familia ya Bakhresa. Namna ambavyo wanaipambania timu yao. Pesa sio kila kitu. Wakati mwingine moyo unahitajika zaidi. Wangekuwa watu wengine Azam ingekuwa IMEKUFA zamani. Wao wanapambana na inafurahisha kuona hata kama hawatwai mataji mara kwa mara, lakini wanaleta ushindani mkubwa.