INAELEZWA kuwa, licha ya kocha Fadlu Davids kuondoka nchini kabla ya kusaini mkataba mpya, mazungumzo yake na bilionea wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji yaliyofanyika juzi kati yameleta neema kwa Fadlu kukubali kurudi sambamba na benchi lote alilofanya nalo kazi msimu uliomalizika.
Chanzo cha ndani kutoka Simba, kimeijulisha Mwanaspoti kuwa, Fadlu pamoja na benchi lote la ufundi wamekubali kusaini mikataba mipya ya mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezwa mwaka mwingine, baada ya kikao kizito kilichowahusisha viongozi wa juu wa klabu hiyo chini ya Mo Dewji.
Hatua hiyo imehitimisha sintofahamu iliyokuwapo juu ya hatma ya benchi la ufundi baada ya kushindwa kufikia mafanikio yaliyotarajiwa msimu uliopita ambapo ilikuwa ni pamoja na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba, benchi lote la ufundi lilikuwa limefikia ukomo wa mikataba yao mara baada ya msimu kumalizika, lakini kutokana na tathmini iliyofanywa kwa kina na viongozi, wakaamua kuwapa muda zaidi kwa imani bado wana mchango mkubwa wa kuipa mafanikio.
Chanzo chetu kilieleza kuwa kulikuwa na minong’ono ya timu kadhaa kutoka ndani na nje ya Afrika ambazo zilikuwa zimeonyesha nia ya kutaka huduma ya Fadlu, jambo ambalo lilimfanya Mo Dewji kuchukua hatua ya haraka kuhakikisha anamsainisha mkataba mpya kabla ya mambo hayajaharibika.
“Mo Dewji hakutaka kusubiri hata kidogo. Aliamua kukamilisha haraka suala la mkataba mpya kwa Fadlu baada ya kuona kuna mawakala wa timu nyingine wakianza kuwasiliana naye. Mo aliamini kuwa licha ya Simba kutotwaa taji msimu uliopita, kazi ya Fadlu inaonyesha dira sahihi ya mafanikio ya baadaye,” kilisema chanzo chetu cha uhakika kutoka ndani ya Simba.
Hii ni mara ya pili kwa Mo Dewji kuingilia moja kwa moja masuala ya kiufundi ndani ya Simba katika kipindi cha hivi karibuni, na mara hii akihimiza utekelezaji wa haraka wa ripoti ya kiufundi iliyowasilishwa na Fadlu kuhusu mabadiliko ya kikosi, falsafa ya timu na aina ya wachezaji awatakao.