Klabu ya Azam FC imethibitisha kumsajili tena Himid Mao Mkami ‘Ninja’, kiungo mkabaji wa kimataifa wa Tanzania, kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao utamuweka katika viunga vya Azam Complex, Chamazi hadi mwaka 2026.
Mao (32) anarejea Azam FC kwa uhamisho huru akitokea klabu ya Tala'ea El Gaish ya nchini Misri, baada ya kuwa nje ya Tanzania kwa kipindi cha takribani miaka 7 tangu alipoondoka kwenda kucheza soka la kulipwa.
Kurejea kwa Himid Mao, ambaye aliwahi kuwa nahodha wa Azam FC na Taifa Stars, kunatajwa kuongeza uzoefu na uimara kwenye safu ya kiungo kuelekea msimu wa 2025/26 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.