Wanjanja Wajipanga Kumtoa Mchezaji Ibrahim Bacca Yanga..



Ubora na nidhamu ya mchezo aliyonayo beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ imetosha kumfanya kocha Mwinyi Zahera kumchomoa nyota huyo kikosini hapo huku akimwambia jambo la kufanya.

Bacca ambaye amekuwa Yanga tangu mwaka 2022 alipojiunga na timu hiyo dirisha dogo msimu wa 2021/22 akitokea KMKM ya Zanzibar, ametengeneza ukuta imara akishirikiana na Dickson Job.

Zahera raia wa DR Congo aliyewahi kuifundisha Yanga, alisema Bacca anapoteza muda kucheza Ligi ya Tanzania kutokana na ubora alionao kwenye eneo analocheza.

Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Zahera alisema Bacca ameonyesha uwezo mkubwa Ligi Kuu, hivyo sasa ni wakati wa kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kwa sababu uwezo na sifa anazo na muda anaoupoteza yatamtokea kama ya Clement Mzize aliyepokea ofa nyingi, lakini hakupata nafasi ya kutoka.

“Mchezaji akiwa na nafasi ya kuondoka Tanzania anatakiwa kuruhusiwa kutoka ili aweze kuongeza uwezo nje na kuja kuitumikia timu yake ya Taifa akiwa ameongeza uzoefu na changamoto mpya kutoka kwa wachezaji wengine wakubwa,” alisema Zahera na kuongeza;

“Kuwazuia wachezaji kwenda kujaribu maisha mengine nje ya timu wanazozichezea ni kuua ubora wa timu ya taifa, mfano mzuri ni Congo wana timu nzuri kwa sababu wana wachezaji wengi wazuri wanaocheza nje ya taifa lao na wamekuwa msaada mkubwa wa ujenzi wa timu bora ya taifa.”

Zahera alisema Bacca ameonyesha ubora katika soka la ndani na bado ana umri unaomruhusu kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania hivyo ni wakati wake kuachwa akasake changamoto nyingine.

Kuhusu Bacca, Zahera anaungana na aliyekuwa kocha wa zamani wa Taifa Stars, Adel Amrouche aliyewahi kusema Bacca ni mchezaji bora Afrika.

“Ubora wa Bacca alionao sasa na nidhamu yake ya mchezo anazidi kuwa mchezaji mkubwa na mimi namuona mbali sana, kwa sasa ukiniambia nikutajie beki bora Afrika jina langu la kwanza ni Bacca,” alisema Amrouche.

Mbali na Bacca, Mkongomani huyo amemtaja kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Pacome Zouzoua anahitaji kujituma zaidi ili kuipa thamani Yanga kutokana na kumuona ni mchezaji aliyekamilika.

Kocha Zahera alisema ni mchezaji aliyekamilika anacheza mpira wa kisasa lakini bado hajaonyesha kile alichonacho ili kuipa Yanga kile walichokitarajia kutoka kwake. “Nafurahishwa na uchezaji wake ni mchezaji mkubwa naweza kusema hivyo kwa sababu anafanya kazi kwa usahihi natamani kumuona akionyesha ubora wake ndani ya timu hiyo aliyopo sasa,” alisema na kuongeza.

Source

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad