Wakati Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema malengo yake ni kumaliza kinara katika Kundi A kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika watani zao, Yanga wanawaza kutoa kichapo katika mechi ya dabi itakayochezwa Oktoba 19, mwaka huu.
Simba imepangwa Kundi A pamoja na CS Costantine ya Algeria, CS Sfaxien kutoka Tunisia na Bravo do Maquis ya Angola.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Fadlu alisema baada ya ratiba hiyo kutoka, ameanza kuandaa mikakati ya kuhakikisha wanafuzu hatua inayofuata mapema zaidi na kuwa kinara kwenye kundi hilo.
Fadlu alisema anajua kundi hilo ni gumu na haitakuwa rahisi kutimiza malengo yake badala yake kazi ya ziada inatakiwa kufanyika.
“Makundi nimeyaona, timu za kundi letu pia nimeziona, pamoja na hayo mipango yetu ni kufuzu mapema zaidi na kuwa vinara ya kundi hili, hatua ya makundi unatakiwa kushinda mechi zako nyumbani, lakini haiwezekani ukafanya hivyo kirahisi kama hujaandaa kikosi, pia mikakati mingi ya kimbinu na kiufundi kuhakikisha unashinda.
Ukweli unabaki pale pale kundi gumu, siku zote ukipangiwa na timu za Afrika Kaskazini ujue umekutana na ugumu, CS Costantine na CS Sfaxien ni timu za Kaskazini, na hili tumeliona wakati tulipocheza dhidi ya Al Ahli Tripoli, lakini nadhani mchezo ule umetupa uzoefu kwa wachezaji ambao walikuwa hawajawahi kukutana na timu za aina ile na mashabiki wake, hivyo watakuwa wameshaanza kuzizoea,” alisema Fadlu.
Kocha huyo alisema wakati wanaendelea na maandalizi ya kuwakabili Yanga, pia wanajipanga na mechi za hatua ya makundi ambapo Novemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wataikaribisha Bravo do Maquis kutoka Angola.
“Haya ni maandaalizi ya jumla, tutacheza dhidi ya Yanga, Oktoba 18, mwaka huu lakini hapo hapo tutakuwa tunaelekea katika mechi ya kimataifa, tutaanza nyumbani na itabidi tushinde ili tuanze kujiamini kuelekea kuongoza kundi letu,” Fadlu alisema.
Wakati huo huo, kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kimeanza rasmi mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa dabi huku wakiahidi wataendeleza vipigo kama kawaida.
Meneja wa Yanga, Walter Harrison, aliliambia gazeti hili baada ya mapumziko ya muda mfupi, wachezaji wa timu hiyo ambao hawakuitwa kwenye vikosi vya timu za taifa walirejea mazoezini ili kujiandaa na mchezo huo muhimu.
“Tulikuwa na mapumziko mafupi, lakini tumerejea tena na hii ni kwa ajili ya wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kuziwakilisha nchi zao katika michezo ya kimataifa, kila kitu kinaenda vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Simba.
Wachezaji waliobaki wanajiandaa vyema ili wenzao wakirejea wote wawe na utimamu wa mwili, programu hii itawapa wanachama na mashabiki wa Yanga kile ambacho tunakitarajia,” alisema meneja huyo.
Aliwataka mashabiki wa Yanga wasiwe na wasiwasi kwa sababu kikosi chao kipo imara na wana matumaini ya kuendelea kuwapa furaha kwa kuendeleza kilio kwa wapinzani wao.
“Hatujawaambia wachezaji wetu wajilinde wakiwa kwenye timu za taifa ili wasiumie wasije kukosa mchezo dhidi ya Simba, hapana, tunataka wapambane kwenye timu zao kwa sababu wakifanya hivyo pia ni sifa kwa Yanga, na inaongeza wigo wa kutoa wachezaji wengi zaidi siku za mbele, sisi tunaamini watarejea salama salmini na kuwahi kucheza mechi hiyo na nyingine bila ya kupata majeraha,” aliongeza meneja huyo.
Yanga kwa siku za karibuni imekuwa mbabe kwa Simba, ikishinda michezo mitatu mfululizo, miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mmoja wa hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni Agosti 8, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ikishinda bao 1-0.
Msimu uliopita wa Ligi Kuu, pia ilipata ushindi michezo yote miwili, ikishinda mabao 5-1, mchezo wa mzunguko wa kwanza na waliporudiana walipata ushindi wa mabao 2-1, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.