Wakati wachezaji wake, Steven Mukwala, Moussa Camara na Valentin Nouma, wakiitwa kwenye timu zao za taifa, Klabu ya Simba inatarajiwa kucheza mechi ya kujipima nguvu nchini dhidi Al Hilal ya Sudan Jumamosi wiki hii, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake wa raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya, huku wakiweka malengo yao ni kufika hatua ya nusu fainali.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema tayari wameshakaa na wachezaji wao na kuwaeleza malengo hayo, licha ya kwamba kikosi chao kina wachezaji wengi wapya.
Alisema pamoja na upya wao, lakini Klabu ya Simba haiwezi kuondoka nje ya malengo yake iliyojiwekea.
"Kwa sasa wachezaji wapo mapumziko, lakini watarejea mazoezini, tutakuwa na michezo kadhaa ya kirafiki, ukiwamo dhidi ya Al Hilal ya Sudan, utakuwa mchezo maalum wa wachezaji kupata ladha ya michezo ya kimataifa, lakini baada ya hapo tutaanza rasmi maandalizi ya mchezo wetu dhidi ya Al Ahly Tripoli.
"Tukishamaliza michezo ya kirafiki, benchi la ufundi litatoa tathmini yake ya kitu gani kinahitajika kabla ya mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Najua tuna kikosi kipya, lakini malengo yetu ni makubwa, yapo pale pale, lengo ni hatua ya juu zaidi ya robo fainali, tumeshakaa na wachezaji tumewaambia, wenzenu huwa wanaishia robo fainali, nyinyi mnatakiwa mvuke zaidi ya hapo na ndicho kilichosababisha majiliwe Simba," alisema Ahmed.
Simba, ambayo ni moja kati ya timu chache Afrika kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho zilizopita moja kwa moja raundi ya kwanza, itaanza mechi yake ya kwanza, Septemba 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Juni 11, nchini Libya dhidi ya timu hiyo, kabla ya kurudiana, Septemba 20, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, wachezaji wapya watatu wa timu hiyo, wameitwa kwenye vikosi vyao vya timu ya taifa kujiandaa na michezo ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, zinazotarajiwa kuchezwa mwakani nchini Morocco.
Straika Mukwala, aliyesaliwa msimu huu, ameitwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes), ambacho kiko Kundi K, kikijiandaa na mechi dhidi ya Afrika Kusini, Septemba 6, ikiwa ugenini, golikipa Camara akiwa ameteuliwa kuunda kikosi cha Timu ya Taifa ya Guinea kilichopo Kundi H pamoja na Timu ya Taifa ya Tanzania, kitakuwa ugenini dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Septemba 6, mwaka huu.
Mwingine ni beki wa kushoto, ambaye, Nouma, akienda kuunda kikosi cha Burkina Faso ambacho siku hiyo hiyo kitakuwa ugenini dhidi ya Senegal, ukiwa ni mchezo wa Kundi L.
Wachezaji wengine watatu wa Tanzania wa timu hiyo, Ali Salim, Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Edwin Balua, wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachotarajia kucheza dhidi ya Ethiopia, Septemba 4, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema licha ya ushindi walioupata kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, bado kikosi chake hakijaanza kucheza soka analolitaka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Fadlu, alisema anaendelea kuingiza mbinu na mifumo yake kwenye timu na anaamini baada ya muda mchache timu hiyo itakuwa moto.
"Nafurahi tumepata ushindi kwenye michezo yetu miwili iliyopita, lakini kwangu bado sijaridhika na kile ninachokitaka, Simba ina nafasi ya kucheza soka la juu zaidi, naamini baada ya muda kikosi kitakuwa na mabadiliko makubwa," alisema Fadlu.
Alisema anaendelea kukiimarisha kikosi na anaridhishwa na kile wanachokifanya wachezaji wake kwenye uwanja wa mazoezi.
"Napenda namna wachezaji wanavyopambana kutafuta namba, ni kitu ambacho nakipenda kwenye kikosi changu, hii itaongeza hali ya kupambana, kwa sasa kazi kubwa kwangu ni kuingiza mfumo na mbinu zangu taratibu, baada ya muda mfupi Simba itacheza mpira mzuri zaidi ya huu," alisema Fadlu.
Alisema anataka kuona kila mchezaji anayepata nafasi ya kucheza anasaidia timu na kutengeneza kikosi kipana.
"Nataka atakayekuwa ndani ni sawa na yule atakayekuwa kwenye benchi, kila mchezaji nataka awe anapata nafasi kulingana na aina ya mfumo nitakaotumia na aina ya mpinzani wetu," alisema Fadlu.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Simba kinatarajia kucheza mchezo wa kirafiki Jumamosi dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuanza kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hizo zote zinatarajia kushiriki mashindano ya Afrika na mchezo huo ni sehemu ya maandalizi yao kabla ya michezo yao ya CAF.
Kocha wa simba, Fadlu, alisema mchezo huo ni kipimo kizuri kwao kuelekea kwenye mchezo wao wa mzunguko wa kwanza hatua ya kwanza dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya.
Simba itaanza kampeni yake kwenye mashindano hayo ya CAF kwa kuanzia ugenini Septemba 13 kabla yakurudiana jijini Dar es Salaam wiki moja baadae ili kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.