Kocha Nabi Atua Makao Makuu Jangwani, Asema "Yanga hii itabeba Ubingwa wa Afrika"

 

Kocha Nabi Atua Makao Makuu Jangwani, Asema "Yanga hii itabeba Ubingwa wa Afrika"

Kocha Mkuu wa Klabu ya kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini, Nasreddine Nabi ameitabiria makubwa Klabu ya Yanga akisema kuwa kwa uwezo walionao wachezaji wao na ubora wa benchi la ufundi, wana uwezo wa kufanya maajabu kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambayo wanashiriki msimu huu.


Nabi amesema hayo leo wakati akihojiwa na wanahabari baada ya kufika katika makao makuu ya Klabu hiyo yaliyopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Mratibu wa Klabu hiyo, Hafiz Saleh pamoja na mashabiki wa Yanga huku kukiwa hakuna taarifa rasmi kuhusu kilichomleta kocha huyo nchini.


Nabi amewahi kuifundisha Yanga kwa misimu miwili na kubeba mataji yaote ya ndani (Ligi Kuu, Shirikisho na Ngao ya Jamii) huku akifanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa kwa sababu ya kanuni dhidi ya USM Alger ya Algeria.


“Naipongeza Yanga kwa kuchukua taji la Ngao ya Jamii. Yanga imekuwa ikiimarika siku hadi siku, ninaiona ni timu ambayo itafanya makubwa kwenye michuano ya Afrika msimu huu hata kuchukua Ubingwa wa Afrika.


“Yanga iko kwenye mikono salama chini ya uongozi wa Rais Eng. Hersi Said, mfadhili wao GSM, hawa watu wanaiweka Yanga kwenye mazingira mazuri ya kiushindani.


“Yanga pia ina kocha mzuri, Miguel Gamondi mwenye uzoefu, kwa hiyo ninaiona ikifika mbali sana katika michuano ya kimataifa,” amesema Kocha Nabi.


Yanga ambayo imeboresha kikosi chake cha msimu uliopita, imeanza vyema msimu huu kwa kuichapa Kaizer Chiefs ya Nabi mabao 4-0 na kutwaa ubingwa wa Toyota Cup, ushindi dhidi ya Simba (bao 1-0) kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii na kutwaa taji hilo la Ngao ya Jamii kwa kuichapa Azam Fc mabao 4-0.


Yanga ambayo msimu uliopita ilifika robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa kwa mikwaju ya penati na Mamelodi, msimu huu imeanza vyema kwenye kampeni ya michuano hiyo kwa kuifunga Vital'O ya Burundi mabao 4-0 kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya awali.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.