Fundi TP Mazembe kutua Yanga

 

Fundi TP Mazembe kutua Yanga

 Fundi TP Mazembe kutua Yanga

Masbingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameendelea kuimarisha kikosi chao kwa kuwanasa nyota wawili wapya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ambao ni beki, Chadrack Boka kutoka Saint Eloi Lupopo na winga wa kulia, Phillipe Kinzumbi wa TP Mazembe, imeelezwa.


Habari kutoka Yanga zinasema wachezaji hao wameshaingia mikataba ya kuitumikia timu hiyo baada ya Rais, Hersi Said, kwenda DRC hivi karibuni kukamilisha mchakato huo.


Chanzo chetu kilisema kuwa Boka atachukua nafasi ya Joyce Lomalisa, ambaye mkataba wake unafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.


Kiliongeza usajili wa Kinzumbi umefanyika kwa haraka kutokana na mahusiano ambayo yamewekwa kati ya Hersi na Mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi.


Chanzo hicho kiliongeza Kinzumbi ataitumikia Yanga huku kukiwa na mazungumzo ya kubadilishana na mshambuliaji Mzambia Kennedy Musonda.


"Dili za wachezaji hao limekamilika, Boka atakuja kuchukua nafasi ya Lomalisa ambaye atapewa mkono wa kwaheri na kutoendelea na Yanga kwa msimu ujao, kuhusu Musonda amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ataenda TP Mazembe akibadilishana na Kinzumbi,” kilisema chanzo chetu.


Taarifa zaidi zilisema uongozi wa Yanga utaendelea kuboresha kikosi chake kwa sababu kinahitaji kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano yote watakayoshiriki.


"Yanga inaendelea kujiimarisha, iko vizuri kumpata kila mchezaji aliye kwenye rada zake na sasa ni muda wa kukamilisha mazungumzo ambayo yalishafanyika huko nyuma, hakuna mchezaji anatesajiliwa kwa kukurupuka," kiliongeza chanzo chetu.


Wakati huo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TP Mazembe, Frederick Kitenge, amewasili nchini kwa ajili ya kukutana na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kufanya mazungumzo mbalimbali ikiwamo suala la maendeleo ya klabu hizo mbili.


Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kuhusu usajili wanaendelea na mchakato huo na watafuata mapendekezo yaliyotolewa na Kocha wao,  Miguel Gamondi.


“Niwaambie mashabiki wa Yanga kwa sasa wanatakiwa kufurahia ubingwa tukiwa na mechi tatu mkononi, suala la usajili mambo mazuri yanakuja na ukizingatia tumeingia ushirikiano na klabu ya TP Mazembe ya DR Congo, viongozi wao wapo nchini kujifunza na kubadilisha ujuzi,” alisema Kamwe.


Naye Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Simon  Patrick, alisema wamepokea 'ugeni mzito' kutoka TP Mazembe wenye lengo la kujifunza mambo mbalimbali ikiwamo  mfumo wa kisasa wa uendeshaji.


“Pia tutakuwa na makubaliano rasmi ya urafiki wa kushirikiana kati ya klabu yetu ya Yanga na TP Mazembe ili kubadilisha ujuzi wa mambo mbalimbali ya kimpira yatakayosaidia timu,” alisema Simon.


Yanga pia inaendelea kukamilisha mchakato wa kusajili wachezaji wake ambao mikataba yao imemalizika au inaelekea ukingoni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.