Yanga yatuma salamu za pole kwa Simba

Yanga yatuma salamu za pole kwa Simba

Uongozi wa Yanga umetuma salamu za pole kwa Simba baada ya ajali iliyotokea na shabiki mmoja wa timu hiyo kufariki dunia.


Alifajiri ya leo shabiki mmoja wa Simba amefariki dunia wakati gari walilokuwa wakisafiria kwenda jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly kupata ajali Vigwaza, Mkoani Pwani.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Yanga na kusambazwa kwenye mitandao yake ya kijamii, uongozi wa timu hiyo umetoa pole na kuonyesha kusikitishwa na kifo hicho na ikiwapa pole pia wale waliopata majeraha.


"Uongozi wa Young Africans Sports Club unatoa pole kwa uongozi wa Simba Sports Club kufuatia msiba wa shabiki wa timu hiyo aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo, kwenye ajali ya gari lililobeba mashabiki, waliokuwa njiani kuja Dar es Salaam kutazama mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


"Tunaomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Marehemu mahala pema peponi. Amen," imesomeka taarifa hiyo iliyotolewa na kitengo cha habari cha timu hiyo.


Pia uongozi huo ulitoa pole kwa wote waliopata majeraha kwenye ajali mbili zilizotokea maeneo ya Vigwaza Pwani na Doma, mkoani Morogoro wapone haraka na kurejea kwenye majukumu yao.


Uongozi wa Yanga pia ulitumia taarifa hiyo kuwataka madereva wote wanaobeba mashabiki kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hizo za Ligi ya Mabingwa Afrika, kuwa watulivu barabarani na kuzingatia alama za usalama wakati wote wa safari.


Simba leo saa 3:00 usiku itavaana na Al Ahly kwenye mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Yanga ikitarajiwa kucheza kesho dhidi ya Mamelodi Sundowns, mechi zote zitapigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.