Mshambuliaji wa Simba, Aubin Kramo amefunguka sababu za kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JNIA kumpokea nyota wa Yanga, kiungo Pacome Zouzoua akidai hiyo ni kawaida na nje ya soka wao ni marafiki wakubwa.
Kramo alionekana jana usiku uwanjani hapo ameambatana na beki wa Yanga, Kouassi Yao na wote walienda kwa ajili ya kumpokea nyota huyo aliyekuwa na timu ya taifa ya Ivory Coast kwa ajili ya mechi za Kirafiki zilizopigwa Ufaransa, dhidi ya Benin na Uruguay ingawa hakupata nafasi kwenye michezo hiyo licha ya kukaa benchi.
Baada ya kusikia maneno mengi kuhusu wawili hao ambao wanacheza timu tofauti za Simba na Yanga, Kramo amesema kuna maisha nje ya soka na wao sio maadui kutokana na timu zao na hakuna wa kuwatenganisha urafiki wao.
Kramo pia amesema alienda uwanjani hapo kwa ajili ya kumpongeza rafiki yake huyo kwa kuteuliwa kwenye kikosi cha Ivory Coast na hayo ndiyo maisha yao.
"Ni kweli nilikuwepo uwanja wa ndege wakati Pacome anawasili, ni rafiki yangu. Nje ya soka tunakuwa pamoja kwani tumetoka nchi moja. Hakuna kinachoweza kunizuia mimi kufanya nilichofanya," alisema na kuongeza;
"Kwanza nilimpokea kama rafiki, pia nilienda kumpongeza kwa kupata nafasi ya kuitwa timu ya taifa letu, hayo ndio maisha yetu nje ya uwanja, hatuwezi kuishi kama tumegombana kisa tunacheza timu mbili tofauti," amesema Kramo.
Staa huyo ambaye anategemewa kuwepo kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi alitua uwanja wa ndege muda mmoja na mastaa sita wa kikosi hicho cha Masandawana waliofika nchini kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakapigwa kesho Jumamosi kuanzia saa 3:00 usiku, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.