Yanga imekubali kichapo kama ilichokipata dhidi ya Ihefu FC katika mzunguko wa kwanza ambapo ilifungwa mabao 2-1 Oktoba 4 na baadaye Azam FC pia wakaifunga 2-1 Machi 17.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema aliamini kuwa na mtihani mgumu kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake baada ya kichapo lakini amekutana na kitu tofauti jana (juzi) baada ya kushangazwa na morali nzuri waliyonayo huku wakisahau matokeo yaliyopita.
"Tumerudi mazoezini jana (juzi) na wahezaji wamekuja na morali nzuri hii imenipa moyo wa kuongeza mbinu zaidi kabla ya kumvaa Mamelodi Machi 30 tukianza nyumbani," alisema na kuongeza.
"Wachezaji wamekiri kufanya makosa na kuahidi kupambana kwa kurudisha furaha ya mashabiki zao kitu ambacho nimekifurahia na naamini kitaongeza chachu ya ushindani kwenye mechi yetu ya Ligi ya Mabingwa Afrika," alisema.
Gamondi alisema baada ya kuona wachezaji wake wamekubali kupoteza na kukubali kuendeleza mapambano tayari kwa mchezo unaofuata amekaa nao na kuwapa namna ambavyo wanatakiwa kufanya ili kuweza kuanza vizuri mchezo wao wa Jumamosi ya wiki ijayo.
NAMNA YA KUTUMIA WACHEZAJI
“Huwa napenda kila mchezaji kwenye kikosi changu kuwa tayari, muda wowote anaweza kutumika kulingana na mahitaji ya mchezo, kila mchezaji kwangu ana nafasi na ndio maana huwa tunawaandaa mazoezini, anayeonakana kufanya vizuri kwenye mpango hupewa nafasi kwa ajili ya timu," alisema na kuongeza;
“Sasa inapotokea mpango wa kwanza umeshindikana ndipo tunaangalia nini kinapaswa kufanyika, je, waliopo wanatosha au tuongeze nguvu kwa mchezaji aliyepo benchi? Vyote hivyo ni vitu vinavyofanyika," alisema Gamondi.
Gamondi ametumia nafasi hiyo pia kuwataka wachezaji wao kuongeza uwajibikaji uwanjani na kujiongeza kimbinu kulingana na mpinzani anapobadili mbinu zake ili kukwepa mitego.
“Hatupaswi kubweteka na kiwango hiki ambacho tumeonyesha, tunatakiwa kufanya zaidi kutokana na uwepo wetu kwenye mashindano ya kimataifa na tuna mchezo mgumu na wa ushindani," alisema.
AUCHO AANZA KUJIFUA
Wakati Yanga ikirudi kwa kuandaa mbinu bora za kuikabili Mamelodi kiungo mkabaji wa timu hiyo Khalid Aucho ameanza mazoezi mepesi chini ya kocha wa viungo ili kumrudisha kwenye ushindani taratibu.
Daktari ya Yanga, Moses Etutu amethibitisha maendeleo ya mchezaji huyo kuwa ni mazuri tofauti na matarajio yao huku akiweka wazi kuwa ni kutokana na namna ya mchezaji huyo alivyo na fikra chanya kwenye mapokeo ya ugonjwa.
Etutu alisema ili kuwaweka wachezaji hao katika hali nzuri na kutokurudi kwenye shida ya kupata majeraha kwa uharaka watalazimika kuwapeleka kwa kocha wa utimamu wa mwili (fitness coach) ili kuwarudisha taratibu kabla hawajacheza mechi za mashindano.
Aucho alifanyiwa upasuaji wa goti hivi karibuni na madaktari wakimkadiria kukaa nje ya uwanja kwa wiki tatu lakini Jumatatu leo ameanza mazoezi mepesi hivyo kocha na mashabiki wa Yanga watarajie kumuona uwanjani kiungo huyo hivi karibuni.