Simba watacheza na Al Ahly ikiwa ni mchezo wao wa kwanza wa Robo Fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kurudiana nao, Aprili 5, 2024 huko nchini Misri.
"Hii leo tumamua kufanya mkutano na wanahabari kwenye Tawi la Simba la Feri hapa sokoni ikiwa ni maalumu na ikiwa kwa mara ya kwanza. Lengo letu ni kufikisha ujumbe tunaokusudia kwamba mechi hii ni kwa ajili ya mashabiki.
“Wanasimba watambue kwamba tunawahitaji sana katika mchezo wa Ijumaa dhidi ya Al Ahly wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kikosi chetu kiliondoka jana jioni kuelekea visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya siku nane ya kujiandaa na mechi hii dhidi ya Al Ahly. Dhumuni la kwenda Zanzibar ni mapendekezo ya mwalimu Benchikha kuhitaji utulivu wa hali ya juu na kufanya mazoezi mara mbili kwa siku ili kutengeneza timu ya kutoa ushindani.
“Lakini pia mwalimu alihitaji kufanya mazoezi usiku, muda ambao mchezo utachezwa ili wachezaji kuzoea mazingiza ya usiku. Kikosi kitakuwa huko hadi wiki ijayo kitakaporudi kwa ajili ya mchezo huo.
“Wengi walitamani mchezo uchezwe saa 10 jioni lakini mechi hizi zinapangwa na watu wengi kwa maslahi ya wengi wakiwepo wenye haki za matangazo na CAF wanaangalia mustakabali wa timu zote mbili. Lakini maslahi mapana ya watu wa imani zote yamezingatiwa na ndio maana ikapangwa muda wa saa 3 usiku ili kila timu na mashabiki wawe katika nafasi nzuri,” alisema Ahmed.