Mchezaji wa zamani wa Taifa Stars na vilabu vya Yanga na Simba, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ amesema kuwa, tofauti na vikosi vya Simba na Yanga kwa sasa ni umri wa wachezaji wao.
Jembe Ulaya amesema kuwa, wachezaji wengi wa Simba umri wao umekwenda kwani wamecheza kwa muda mrefu hivyo inatakiwa damu changa kwa ajili ya kupambana zaidi huku akidokeza kuwa, wenzao yanga waliliona hilo mapema ndiyo maana wakasajili wachezaji vijana ambao wanaonekana kupamabana uwanjani kuliko watani zao.
“Tofauti kati ya wachezaji wa Simba na Yanga ni umri, ukitazama wachezaji wengi wa Simba umri wao ni kama umeenda, lakini kwa Yanga umri wao bado unawalipa. Wanaweza kupambana na wakiongezewa wachezaji wazuri wanaweza kufanya viuzuri kwa misimu inayokuja.
“Simba waongeze wachezaji vijana ambao wanaweza kupambana kwa miaka mine mitano inayokuja bila kuwa na mashaka yoyote,” amesema Jembe Ulaya.