Viongozi wa Simba Kumleta Mwamba Huyu Hapa Kuchukua Nafasi ya Kocha Robertinho

 

Viongozi wa Simba Kumleta Mwamba Huyu Hapa Kuchukua Nafasi ya Kocha Robertinho

MABOSI wa Simba juzi jioni walijifungia kwa saa kadhaa jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali na mwishowe wakaibuka na jina la Kocha Mtunisia, Radhi Jaidi na wanaendelea kumjadili kuchukua nafasi ya Roberto Oliveira ‘Robertinho’ baada ya kuamua kuachana na Abdelhak Benchikha kwa sababu ya dau.

Dau ya kocha huyo Mualgeria ambalo ni zaidi ya Sh500 milioni, limewafanya mabosi wa Simba kuingia ubaridi na ndipo wajumbe wakaibuka na jina la Jaidi ambaye ana cv kubwa katika soka la Afrika kama ilivyo kwa Benchikha na kama mambo yataenda vizuri huenda kocha huyo Mtunisia akatua Simba.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa kutoka ndani ya Simba ni kwamba viongozi wamemgeukia Jaidi ambaye inaelezwa kama mambo yataenda sawa basi atatangazwa kuiongoza timu hiyo kabla ya mchezo na ASEC Mimosas utakaopigwa Novemba 25 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Ni moja ya makocha wanaopewa nafasi kubwa sana ya kupewa timu, ingawa mchakato umekuwa mgumu kwa sababu kila anayeletwa mezani kwetu amekuwa na mahitaji makubwa ambayo sisi viongozi tunashindwa kukubaliana nayo,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya kikao hicho ya Simba.

Hatua ya kutua kwa kocha huyo inajiri baada ya makocha waliopendekezwa mwanzoni kuonekana ngumu kuwapata kutokana na kuhitaji masilahi makubwa ya kuwalipa jambo lililowafanya mabosi hao kuangalia njia nyingine ya kutatua changamoto hiyo.

Makocha waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ni, Abdelhak Benchikha aliyeachana na USM Alger ya kwao Algeria kufuatia kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita baada ya kuifunga Yanga pia akichukua Super Cup akiifunga Al Ahly.

Wengine ni Nasreddine Nabi anayeifundisha FAR Rabat ya Morocco na Sven Vandenbroeck aliyewahi pia kuifundisha timu hiyo ingawa licha ya kutokuwa na kibarua chochote kwa sasa baada ya kuachana na CR Belouizdad ila imeonekana ngumu kurejea.

Mapema hivi karibuni, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally akizungumzia suala la kocha mpya alisema wapo makocha wengi waliotuma maombi ya kupewa nafasi hiyo ingawa viongozi wanaendelea kushughulikia na muda wowote wataweka wazi itakapokamilika.

“Niwatoe hofu mashabiki zetu kuhusu suala la kocha, viongozi wapo makini kulifanyia kazi na siku sio nyingi mtaona tukiweka wazi, lengo la kuchelewa ni kutokana na kujiridhisha kwa kina kwa wale wote waliotuma maombi yao,” alisema Ally.

JAIDI NI NANI?

Jina kamili la kocha huyo ni Radhi Ben Abdelmajid Jaidi aliyezaliwa Agosti 30, 1975, nyota wa wa zamani wa Tunisia akicheza beki wa kati akianzia soka la vijana akiwa na Stade Gabesien na Esperance zote za Tunisia kati ya 1988-1993 kabla ya kuichezea Esperance ya wakubwa kati ya 1993-2004 na kutua Bolton Wanderers, Birmingham City na Southampton zilizowahi kutamba Ligi Kuu ya England kisha kugeukia ukocha na kuanza 2013 na kufundisha timu za vijana ya Southampton za U21 na U23 kati ya 2014-2017.

Kocha huyo mwenye leseni ya UEFA Pro, anaopenda kutumia mfumo wa 4-3-3 amewahi pia kuwa Kocha Mkuu wa Hartford Athletic inayoshiriki Ligi ya Marekani (USL Championship) huku akiwa pia kocha msaidizi wa timu ya Cercle Brugge ya Ubelgiji kabla ya kutua Esperance ya Tunisia alioachana nao mwaka jana akitoka kuwapa taji la Super Cup kwa kuifunga CS Sfaxien.

Enzi za uchezaji Jaidi alinyakua mataji 18 tofauti yakiwamo ya Ligi Kuu Tunisia na ile ya michuano ya CAF akiwa na klabu tofauti zikiwamo zile zilizowahi kutamba Ligi Kuu ya England, zikiwamo Bolton Wanderers Birmingham City na Southampton aliyoichezea hadi 2012. kabla ya kugeukia ukocha ambapo ametwaa taji moja tu la Super Cup akiwa na Esperance.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad