Kocha Mpya Simba Apewa Faili La Robertinho

Kocha Robertinho

 Kocha Mpya Simba Apewa Faili La Robertinho

UONGOZI wa Simba, umevunja ukimya na kueleza sababu ya kutaka kupata kocha aliye bora ambaye watakuwa naye kwenye mipango ya muda mrefu.


Hali hiyo imetajwa ndiyo sababu ya kuchelewa kumtangaza mrithi wa Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kwani wanataka kocha ajaye, afanye zaidi ya kile kilichofanywa na mtangulizi wake.


Awali Simba walisema wiki iliyopita watamtangaza kocha mkuu pamoja na wa viungo, lakini imeshindikana, huku wakiendelea na mchakato wa kupitia baadhi ya wasifu za makocha walioomba kurithi mikoba ya Robertinho.


Baadhi ya makocha wanaohusishwa kuchukua nafasi ya Robertinho ndani ya Simba ni Sven Vandenbroeck na Abdelhak Benchikha.


Akizungumza na Spoti Xtra, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema hawataki kufanya jambo hilo kwa haraka kwa sababu wanahitaji kufanya maboresho makubwa kwa kuleta mtu ambaye wataenda nao sawa kwenye mipango yao ya muda mrefu.


Alisema wanahitaji kuwa watulivu katika mchakato huo wa kupata mtu aliyekuwa sahihi ambaye atakuja kwa ajili ya kwenda nao njia moja kuhakikisha wanapata kocha bora mwenye vigezo walivyoweka.


“Tumeona kuna makocha wengi wakitajwa akiwemo Benchikha, ni kocha mzuri, hakuna sehemu viongozi wa Simba wamemtaja, mchakato umechelewa kwa sababu ya kutohitaji kupata kocha baada ya mechi mbili tunamuondoa.


“Kuepukana na hilo, tumelazimika kuwa makini katika mchakato huu, mashabiki wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa sababu viongozi wanapambana kutafuta mtu sahihi wa kuja kuchukua nafasi ya Robertinho,” alisema Ally.

STORI NA IBRAHIM MUSSA


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.