Majeraha Haya Yanamweka nje Haaland?

 

Majeraha Haya Yanamweka nje Haaland?

Mwisho mwa wiki iliyopita na wiki hii kulikuwa na mapumziko ya Ligi Kuu mbalimbali duniani kwa ajili ya kupisha mechi za kimataifa zikiwamo zile za kuwania kufuzu ushiriki wa fainali za Euro 2024 zitakazochezwa nchini Ujerumani.


Kama ilivyo kawaida kwa wachezaji mastaa ndio kipindi chao cha kuacha majukumu ya klabu na kwenda katika majukumu ya kimataifa katika timu zao za Taifa.


Mmoja wa mastaa hao ni pamoja na Erling Haaland ambaye amepata majeraha ya kifundo katika mchezo wa kirafiki wakati akiwa na timu yake ya taifa ya Norway.


Alikutana na majanga hayo siku ya alhamisi usiku wiki iliyopita katika mchezo wa kirafiki dhidi timu ya taifa ya Kisiwa cha Faroe kwa lengo la kujiandaa na mchezo wa Jumapili wa Euro dhidi ya Scotland.


Katika mchezo huo walioshinda 2-1 alichezewa faulu iliyomfanya kugaragara chini kwa maumivu huku akishikilia kifundo cha mguu wa kushoto jambo ambalo lilileta hofu pengine amepata jereha kubwa.


Ingawa alipata majeraha hayo aliweza kumaliza mchezo huo hadi mwisho lakini baadaye alipatwa na maumivu makali hali iliyolazimu kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.


Jumamosi iliyopita, daktari wa timu ya Norway, Ola Sand aliweka wazi utimamu wa Halaand kwa kueleza kuwa mchezaji huyo alipata majeraha ya kifundo cha mguu wa kushoto.


Alieleza majeraha hayo hayakuwa makubwa kama ilivyodhaniwa awali, lakini yalimpa maumivu makali kiasi cha kuzuia ufanyaji kazi wa mguu eneo la kifundo.


Tatizo hilo ndio lilisababisha kutojumuishwa katika mchezo wa Jumapili wa kusaka tiketi ya Euro 2024 waliotoka mabao 3-3 dhidi ya Scotland.


Daktari huyo alifafanua kuwa alipata majeraha ya ndani kwa ndani ya tishu laini na hakuwa na mvunjiko wowote katika eneo la kifundo cha mguu huo.


Ukiacha pengo lake hilo katika timu yake ya taifa ambayo haina uhakika wa kukata tiketi, kwa upande wa klabu yake ya Manchester City tayari kocha Pep Guardiola amestushwa na taarifa hiyo.


Sababu ni kutokana na klabu hiyo hapo keshokutwa Juamosi ina mchezo mgumu wa Ligi ya EPL dhidi ya Liverpool ambayo ni ya pili katika msimamo wa ligi, pointi moja nyuma ya Man City wanaongoza ligi.


Mshambuliaji huyu mwenye miaka 23 ambaye mtaani wanamwita mtambo wa mabao tayari msimu amefunga 13 ya EPL katika mechi 12 alizocheza.


Inaelezwa nafasi ya kucheza mchezo huo wa Jumamosi ni ndogo sana kwani bado ana maumivu ambayo ni ishara kuwa bado hajakuwa timamu kuweza kupona na kucheza mechi hiyo.


Ingawa katika soka na utabibu wa kisasa lolote linaweza kujiri kwani kwa mujibu wa chama cha soka cha Norway inaonyesha hayakuwa majeraha makubwa.


Hii ni mara ya pili kupata jeraha la kifundo katika mguu huo huo, itakumbukwa mwezi uliopita alipindisha vibaya kifundo katika mchezo wa EPL walioshinda mabao 6-1 dhidi ya Bournemouth.


Kupata jeraha jingine katika mguu huo huo kunaongeza hatari ya kupata majeraha ya kujirudia hatimaye kuwa tatizo sugu linaloweza kumweka nje mara kwa mara.


Uchunguzi ambao ni kawaida kufanyika kwa mastaa kama hawa wanaocheza ligi za kulipwa ni pamoja na kipimo cha MRI ambayo ndicho kinaonyesha kwa kina majeraha ya tishu laini kama ligamenti.


Sababu za majeraha ya kifundo kuchelewa kupona


Eneo hili la kifundo lina matumizi mengi katika soka kwani ndilo linalohusika na matendo mengi ikiwamo kupiga mashuti, kukimbia, kuruka, kupiga chenga, kukaba na kukwatua.


Kutokana na kuwa na kazi hizo eneo hili linajikuta linakuwa katika hatari ya kupata majeraha mara kwa mara. Majeraha yake yanaweza kuwa ya kawaida, wastani, makubwa na makubwa sana.


Ni kawaida kuchukua muda mrefu kupona kutokana eneo hili kuwa na tishu mchanganyiko ikiwamo tishu ngumu kama vile vijifupa vya funiko la mguu na vidole, kisigino na vijifupa plastiki na mifupa inayounda ungio la kifundo linalojumuisha mifupa miwili ya mguu.


Vile vile na tishu laini ambazo ni nyuzi za tendoni ambazo ni miishilio ya misuli inayojipachika katika mifupa na nyuzi ngumu yaani ligamenti ambazo zinaunganisha mifupa na mwingine.


Sababu kuu ya kitabibu inayochangia majeraha ya kifundo kuchelewa kupona ni kutokana na kiasi kidogo cha damu kinachotirirka katika nyuzi za ligamenti na tishu nyingine za kifundo.


Ndio maana pale yanapotokea majeraha makubwa mpaka makubwa sana huwa ni kawaida kwa majeraha hayo ya kifundo kuchukua miezi 3-6 kupona kabisa.


Wakati huo huo, eneo hili linapata shinikizo kubwa la uzito wa mwili wakati nyayo inapokuwa inakanyaga ardhi, hii inaliweka eneo hili kupata majeraha kirahisi na kuchelewa kupona.


Pata picha picha uzito wa Haaland ni kilo 75 na huku akiwa na urefu wa mita 1.78, ni mshambuliaji ambaye ana kasi na anapiga mashuti mara kwa mara na huku akikabwa na mabeki wanaomkwatua.


Namna ya kupunguza majeraha ya kifundo


Utimamu wa mchezaji unategemea zaidi mazoezi ya kujenga mwili na viungo, unywaji maji na kula vyakula vinavyoshauriwa wataalam wa lishe za wanamichezo, kulala na kupumzika masaa 8-10 kwa siku.


Vile vile kuwa na nidhamu na mienendo na mitindo bora ya kimaisha ikiwamo kutojihusisha na ulaji holela wa vyakula, matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi na dawa za kulevya.


Ni muhimu mchezaji kupasha mwili moto na kunyoosha viungo vya mwili kwa kuzingatia mazoezi sahihi yanayoelekezwa na walimu wataalam wa mazoezi ya viungo kabla na baada ya mechi au mazoezi.


Mazoezi haya yanasaidia viungo kuwa na utayari wa juu, kulainika taratibu, kuimarika na kunyumbulika kwa hali ya juu kwa maungio wakati wa kucheza.


Kuepuka kucheza kabla ya jeraha kupona au kucheza huku bado ana maumivu. Vile vile kutotumia kiholela dawa za maumivu ambazo baadhi hununua binafsi pasipo kushauriwa na daktari.


Chukua hii


Mchezaji aliyepata jeraha la kifungo kifundo apate matibabu ya awali ya huduma ya kwanza ikiwamo kupumzishwa, kuwekewa barafu dakika 10-15 katika jeraha, kufunga bandeji mvutiko na ibane kiasi na kuunyanyua mguu kuzidi kifua wakati wa kulala.


Muhimu kushikamana na ushauri unaotolewa na wataalam wa Afya wakati unapokuwa majeruhi.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.