Za Ndanii Kabisa, Didier Gomes Kurudi Tena Tanzania, Mpingo Yote Iko HiVi

 


Uongozi wa Singida Fountain Gate FC, umekamilisha makubaliano na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Didier Gomes, kuja kukinoa kikosi cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Gomes alionekana Misri Jumapili (Oktoba Mosi) kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Future FC na Singida Fountain Gate FC, akiwa miongoni mwa watazamaji walioko jukwaani.

Taarifa za uhakika zinaeleleza kuwa, tayari Gomes amekubaliana na uongozi wa Singida Fountain Gate FC na muda wowote atasaini mkataba wa kukinoa kikosi hicho katika michezo ya Ligi Kuu na michuano mingine.

Chanzo cha habari hizi kimeeleza kuwa uongozi umeona Gomes anastahili kuja kuchukuwa nafasi ya Ernest Middendorp aliyeondoka kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri na waajiri wake na timu kuwa chini ya Mkurugenzi Ufundi, Ramadhan Nsanzwirimo.

“Mazungumzo yamekamilika kichobakia ni kusaini mkataba na kumtambulisha rasmi kwa sababu timu ilipokuwa Misri, Gomes alikuwapo akiangalia mchezo huo ili kuangalia timu yake hiyo mpya kabla ya kuanza kuinoa,” kimeeleza chanzo cha habari hii.

Afisa Habari wa Singida Fountain Gate FC, Hassan Masanza, amekiri kuwapo kwa mazungumzo na baadhi ya makocha akiwamo Gomes kwa ajili ya kuona nani anakuja kuwa kocha mkuu.

“Kila mtu anaelewa nafasi ya kocha mkuu ipo wazi na viongozi wako kwenye mazungumzo na makocha mbalimbali, kikubwa tunaangalia mwalimu anayeifahamu soka la Tanzania na atakayeweza kutupelekea kimataifa kwa msimu ujao,” amesema Masanza.

Ameongeza kuwa baada ya kufanikiwa kumpata kocha wanayemhitaji na kufika vigezo vyao, wataweka wazi na kwamba kwa sasa timu inaendelea kuwa chini ya Nsanzwirimo hadi hapo atakapopatika kocha mkuu.

Kikosi cha Singida Fountain Gate FC, tayari kimewasili Manungu, Turiani mkoani Morogoro kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa kesho Alhamis (Oktoba 05) katika Uwanja wa Manungu Complex.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.