Washambuliaji Bado ni Tatizo Ligi Kuu

Washambuliaji Bado ni Tatizo Ligi Kuu

 Washambuliaji Bado ni Tatizo Ligi Kuu

Makocha wa timu tano za Ligi Kuu wana kazi kubwa ya kuimarisha safu zao za ushambuliaji kutokana na ubutu zinazondelea kuonyesha katika mashindano hayo msimu huu.


Timu hizo tano ni Singida Big Stars, Coastal Union, Namungo, Kagera Sugar na Dodoma Jiji.


Hadi sasa wakati Ligi hiyo ikiwa imefikisha raundi tano, timu hizo kila moja imepata bao moja tu kutoka kwa wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji, huku mengine yakitoka kwa nyota wa nafasi nyingine.


Na ubutu huo wa washambuliaji umeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa timu hizo kufunga idadi ndogo ya mabao na hata kukusanya pointi kiduchu kulinganisha na mechi ilizocheza.


Coastal Union na Namungo ndiyo zenye hali mbaya zaidi, kwani kila moja imefunga mabao mawili katika mechi tano ilizocheza na bao moja kwa kila timu likiwa limefungwa na mshambuliaji na mengine yakipachikwa na viungo.


Timu nyingine iliyofunga mabao mawili ni Geita Gold, lakini yenyewe angalau mabao yote hayo yamewekwa kimiani na mshambuliaji ambaye ni Elias Maguli.


Singida Big Stars na Kagera Sugar, kila moja imefunga mabao tatu katika mechi tano, lakini kati ya hayo matatu ni moja tu limefungwa na mshambuliaji.


Mabao mawili ya Singida yamefungwa na viungo, wakati kwa upande wa Kagera Sugar, bao moja lingine limefungwa na beki na moja limepachikwa na kiungo.


Timu nyingine ambayo washambuliaji wake wanahaha ni Dodoma Jiji ambayo licha ya kupachika mabao manne hadi sasa, ni moja tu lililofungwa na mshambuliaji na moja likipachikwa na kiungo na lingine beki huku bao moja likiwa la kujifunga la wapinzani.


Ihefu SC ni timu nyingine inayohangaishwa na ukame wa mabao ambapo imefunga mabao matatu tu, kati ya hayo mawili yakifungwa na washambuliaji na moja likipachikwa na beki.


Washambuliaji wa Mashujaa nao wanasuasua japo wamepachika mabao mawili hadi sasa kwani timu yao imepachika mabao manne tu hadi sasa, idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na mechi walizocheza.


Yanga ndio timu ambayo licha ya washambuliaji wao kutokuwa na makali, imefunga idadi kubwa zaidi ya mabao ambayo ni 15 na imekuwa ikitegemea zaidi viungo wake ambao wamefunga mabao 11 huku washambuliaji wake wakipachika mabao mawili tu na mengine mawili yakiwa ya mabeki.


Timu yenye washambuliaji tishio zaidi ni Simba ambayo hadi sasa, kati ya mabao 14 iliyopata, washambuliaji wake wamefumania nyavu mara 9 huku matano yakifungwa na viungo.


Kocha msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Liogope alisema kuwa watatumia muda wa mapumziko ya ligi kunoa safu yao ya ushambuliaji.


"Ni kweli tunahitaji kufunga mabao na hatujawa vyema katika mechi hizi ambazo tumeshacheza lakini bado kuna michezo 25 mbele. Jukumu letu kama benchi la ufundi ni kufanyia kazi hilo na naamini katika kipindi hiki ambacho ligi inasimama, tutaimarisha eneo hilo," alisema Liogope.


Mshambuliaji wa Coastal Union, Hija Ugando alisema ugumu wa ligi umechangia kuwapa ukame wa mabao, lakini watajirekebisha siku za usoni.


"Ushindani umekuwa mkubwa na timu zinajipanga sana kimbinu hivyo inaleta ugumu lakini hilo halipaswi kuwa jambo la kujitetea. Kitu cgha muhimu ni kuzidi kujituma mazoezini na katika mechi naamini mabao yatakuja tu," alisema Ugando.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.