Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limethibitisha tukio la mauaji lililotokea jana jioni Septemba 16, 2025 saa 12:50 katika Kitongoji cha Ululu, Kata ya Idiwili, Wilaya ya Mbozi ambapo Evaristo Zabroni Mwambogolo (28) Mkulima wa eneo hilo alichomwa kisu kifuani na kufariki dunia wakati akipelekwa Zahanati ya Lyula kwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, chanzo cha ugomvi huo ni mabishano makali kuhusu ushabiki wa Timu za Simba na Yanga na inadaiwa Evaristo na Exavery Jamsoni Mwaweza walianza kubishana kuhusu ubabe wa Timu hizo hali iliyopelekea Mtuhumiwa Exavery kuchomoa kisu alichokuwa nacho na kumjeruhi Evaristo sehemu ya moyo.
Mtuhumiwa alitoroka kusikojulikana baada ya tukio hilo ambapo tayari Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali kuhakikisha anakamatwa ili kufikishwa kwenye Vyombo vya sheria huku pia uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Kamanda wa Polisi Mkoani humo ametoa wito kwa Wananchi kuepuka mabishano yenye hisia kali hasa yanayohusu Timu za Simba na Yanga akisisitiza kwamba upendo wa michezo haupaswi kugeuka chachu ya vurugu