Dar es Salaam, Julai 10, 2025 – Kipa namba moja wa klabu ya Yanga SC, Djigui Diarra, anaendelea kuwa gumzo kwenye soko la usajili baada ya taarifa kuibuka kuwa baadhi ya timu zinafuatilia kwa karibu saini yake, huku uongozi wa Yanga ukisisitiza kuwa bado wana mpango naye.
Diarra, ambaye alikuwa chaguo la kwanza chini ya kocha Miloud Hamdi, alicheza mechi 23 kati ya 30 msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, akicheza jumla ya dakika 2,070. Katika mechi hizo, alifungwa mabao 8 pekee, akionyesha kiwango cha juu cha kuaminika langoni.
Kwa ujumla, Yanga SC ilicheza mechi 30 msimu huu na kuvuna pointi 82 katika dakika 2,700, na kutwaa taji la ligi kwa mara ya 31 katika historia yake. Djigui alikosekana kwenye mechi 7 tu msimu mzima.
Kipa huyo raia wa Mali amekuwa mfano bora kwa makipa wa ndani kutokana na uwezo wake wa kutoa maelekezo uwanjani, utulivu mkubwa langoni, pamoja na pasi za uhakika anazopiga — sifa ambazo zimeongeza ushindani miongoni mwa makipa wa ligi ya Tanzania.
Kumekuwa na uvumi unaodai kwamba huenda Diarra akatimka Yanga, lakini Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amefunguka na kusema hakuna mpango wa kumwacha aondoke kwa sasa.
“Diarra ni kipa bora na yeye mwenyewe anajua. Ikiwa angetaka kuwa na hati safi zaidi ya 17 alizonazo alikuwa na nafasi ila aliamua mwenyewe. Bado tuna mpango naye, hivyo yupo sana ndani ya kikosi cha Yanga SC,” alisema Kamwe.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo taarifa za tetesi za usajili zikimhusisha Diarra na vilabu kadhaa nje ya nchi, huku wachambuzi wa soka wakiona kuwa nafasi ya kipa huyo kwenye kikosi cha Yanga bado ni muhimu.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu itazinduliwa rasmi Julai 24 2025 usipange kukosa.