Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) linafikiria kufuta muda wa ziada (extra time) kwenye michezo ya mtoano ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo ikiwa mchezo wa mtoano wa UEFA Champions league utamalizika kwa sare baada ya dakika 90 za nyumbani na ugenini basi mikwaju ya penalti itafuata tofauti na utaratibu wa kawaida wa dakika 30 za nyongeza ili kumpata mshindi.
Mabadiliko haya yatakayoanzia hatua ya 16 bora yanalenga kupunguza uchovu kwa wachezaji huku timu nyingi zikikabiliwa na mwingiliano wa ratiba ya mashindano ya nyumbani, mashindano ya Ulaya na kupanuka kwa michuano ya Kombe la Dunia la Vilabu msimu huu.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yanaweza yasianze kufanya kazi mapema kutokana na mkataba wa haki za televisheni kati ya UEFA na washirika wake wa kibiashara ambao utakafikia ukomo mwaka 2027 ingawa mabadiliko yanaweza kutokea ikiwa kutakuwa na mashauriano zaidi kati ya pande hizo mbili.