WAARABU WAMLETA KOCHA MICHO DAR KISA SIMBA

 

Waarabu Wamleta Kocha MICHO Dar Kisa Simba.....

Simba imeingia kambini tangu jana jijini Dar es Salaam tayari kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwa inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kutinga hatua hiyo.


Milutin Sredojevic ‘Micho’


Lakini je unamkumbuka Milutin Sredojevic ‘Micho’, kocha wa zamani wa Yanga aliyeweka rekodi na klabu kadhaa katika michuano ya CAF? Jamaa ametua nchini na kinachoelezwa ni kwamba Micho aliyewahi pia kuinoa St George ya Ethiopia atakuwa nchini akikatiza mitaa ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo moja tu - kuibeba timu iliyomleta.


Simba kwa soka ililopiga jijini Tripoli limewashtua Walibya walioamua kumbeba Micho ili aje kuwabeba katika mechi ya Dar.


Mwanaspoti inafahamu alfajiri ya leo Alhamisi, Al Ahli ilitarajiwa kuwasili nchini ikiwa na Micho kwa ajili ya kuisaidia timu katika mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni, kutokana na rekodi alizonazo na pia kuwahi kufundisha Yanga na timu kadhaa za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Kiungo wa Simba, Yusuf Kagoma akigombea mpira na mchezaji wa Al Ahli Tripoli katika mchezo uliopigwa Jumapili iliyopita mjini Tripoli, Libya.


Micho kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Libya, lakini atakuwa sehemu ya msafara wa Al Ahli, japo mabosi wa klabu hiyo wamegoma kufafanua zaidi juu ya ujio wa kocha huyo aliyeinoa Yangha mwaka 2007, lakini Mwanaspoti linafahamu kocha huyo amepewa kazi maalum ya kuwasaidia makocha wa timu hiyo juu ya kujua mambo mazito ya Wekundu hao.


Al Ahli Tripoli imechukua uamuzi huo baada ya kuona mziki mzito wa Simba walipocheza nyumbani kwao Jumapili iliyopita matokeo yakiwa 0-0, wakasema lazima waongeze nguvu ili mambo yasiharibike wakija ugenini.


Katika kuangalia nani ni mtu sahihi wa kuwasaidia, moja kwa moja wakatua kwa Micho wakiamini ana mambo manne yatakayowasaidia kutoboa hatua ya makundi.


“Micho ameongezwa katika msafara wa timu inapokuja hapo Tanzania, hapa Libya kila mtu alitarajia tungefanya vizuri kwenye mechi ya nyumbani, lakini ikawa tofauti, hivyo tunaamini kocha huyu kwa sababu analijua soka la Afrika Mashariki atakuwa msaada mkubwa,” amesema mmoja wa mabosi wa juu wa Shirikisho la Soka la Libya.


Wakati Al Ahli Tripoli wakiendelea na mikakati hiyo, kumbuka pia wamemwambia kocha wao, Chokri Khatoui akirudi Libya mkononi awe na tiketi ya timu kucheza makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, la sivyo atafute njia yake mapema.


Al Ahli Tripoli inaamini kutokana na kikosi chao kujaa nyota wa maana kama Hamdou Elhouni, Moayed El Lafi, Sand El Warfali, Ahmed Karaoua, Mohamed El Mounir, Ghilan El Shaalali, El Jazouli Noah na Agostinho Cristovao Paciencia ‘Mabululu’, basi hawana sababu ya kushindwa kufuzu makundi.


Uamuzi wa Waarabu hao kumwongeza Micho katika mikakati yao kuja kuikabili Simba umebeba jumla ya mambo haya manne.


UYANGA WAKE Kwa namna ambavyo Micho amekuwa na uhusiano mzuri na watu wa Yanga, kwani aliishi nao vizuri kipindi anafundisha hapo, inaweza kuwa rahisi kwake kupata chochote kitu kuhusu kuuendea mchezo huo dhidi ya Simba ambao ni wapinzani wa jadi wa klabu yake ya zamani.


Hiyo inatokana na namna mashabiki wa Simba na Yanga walivyo, ule ushindani wao wa ndani umepenya hadi kimataifa, licha ya kwamba kumekuwa na wimbo wa kuwa wazalendo kwa ajili ya Watanzania kuzisapoti timu za hapa nyumbani bila ya kujali itikadi ya ushabiki pindi linapokuja suala la michuano ya kimataifa, lakini kwa namna moja ama nyingine haipo hivyo.


Mara kadhaa imeshuhudiwa mashabiki wa upande mmoja wakiisapoti timu ya nje inapokuja hapa nchini kucheza dhidi ya mwenzake kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimekuwa kikiwaaidisha wageni.


USHAWISHI KWA WACHEZAJI Inaelezwa Micho ni aina ya makocha wenye ushawishi mkubwa kwa wachezaji anaofanya nao kazi, akiwaambia leo lazima tufanye hivi, basi inafanyika hivyo na hakuna anayerudi nyuma.


Kitu hicho amekuwa nacho katika timu zote anazofundisha hivyo Al Ahli Tripoli wanaona baada ya kupata suluhu nyumbani ni kama morali ya wachezaji imeshuka, hivyo wanamtumia Micho kuirudisha hali yao ya upambanaji.


UZOEFU AFRIKA MASHARIKI Inafahamika, Micho amewahi kufundisha soka Ukanda wa Afrika Mashariki tangu 2002 hadi 2023 na amezinoa klabu mbalimbali na timu za taifa.


Akiwa anafundisha katika Ukanda wa Afrika Mashariki, anazijua tabia za wachezaji na hata viongozi wa timu pindi wanapojiandaa na mechi hasa zile zenye umuhimu mkubwa.


Rekodi zinaonyesha mwaka 2002 hadi 2004, Micho alikuwa Kocha wa SC Villa ya Uganda kisha 2004-2006 akaifundisha Saint-George ya Ethiopia ambayo nayo ipo Ukanda wa soka wa Cecafa.


Mwaka 2007 alikuwa Yanga kwa muda mfupi kabla ya kurejea Saint-George alipokaa nao 2007 hadi 2010. Hakuishia hapo kwani mwaka 2010 hadi 2011 aliifundisha Al-Hilal Omdurman ya Sudan na 2011 hadi 2013 akapewa kikosi cha timu ya taifa ya Rwanda, kisha Uganda 2013 hadi 2017 na 2021 hadi 2023.


Kuzunguka katika timu zote hizo za Ukanda wa Cecafa kunampa nafasi kubwa Micho kulifahamu vizuri soka la Afrika Mashariki hivyo anajua nje ndani mbinu zinazofanyika.


MAFANIKIO CAF Ukiachana na kulifahamu soka la Afrika Mashariki, Micho amefanikiwa kwa kiasi chake katika michuano ya CAF. Mwaka 2010, Micho aliiongoza Al-Hilal ya Sudan kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kitu ambacho anajivunia mpaka sasa.


Kwa kuonyesha hakubahatisha, mwaka uliofuatia 2011 akiwa bado ni kocha wa Al Hilal, akacheza tena nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakatolewa na CS Sfaxien ya Tunisia kwa penalti baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1.


Kucheza nusu fainali mbili na timu moja katika michuano miwili tofauti mikubwa ngazi ya klabu barani Afrika, inaonyesha Micho ni kocha mzoefu wa michuano hiyo.


Hivyo katika kuhakikisha Al Ahli Tripoli inafuzu angalau makundi, imeona kupitia mambo hayo basi Micho ni mtu sahihi kuongeza nguvu kikosini kwao.


Ukiachana Micho kushuka na timu hiyo, lakini Mwanaspoti linafahamu maofisa wa Al Ahli Tripoli ambao walitua kwa siri na ndege waliyorudi nayo Simba alfajiri ya jana Jumatano, wanafanya mawasiliano ya kila kitu na kocha huyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad